Aussems: Januari tunaanza upya wasee

HADI Ligi Kuu Kenya inachukua mapumziko ya takribani wiki mbili, AFC Leopards haijakuwa na mwanzo mzuri wa msimu mpya 2022/23 ikishinda mechi moja kati ya tano walizocheza wakiambulia sare mbili na kupoteza michezo miwili.
Hata hivyo kocha wa Ingwe, Patrick Aussems, amewatuliza presha ya mashabiki baada ya kuona timu yao ikiwa nafasi ya tisa na pointi tano kuwa mambo mazuri yanakuja.
Mashabiki wa Ingwe waliyojikusanya baada ya mechi yao ya mwisho Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi uliyoishia sare tasa dhidi ya Kakamega Homeboyz, walimuita nahodha Eugene Mukangula na kumpasha.
Aussems amefichua ameiona ghadhabu ya mashabiki na kuahidi kubadilisha mambo huku akisisitiza msimu wao unaanza upya Januari 4 mwakani mechi za FKFPL zitakaporejelewa.
“Ninachoweza kusema ni kwamba msimu wetu unaanza Januari sababu tutakuwa na wachezaji zaidi kuliko ilivyosasa, hilo la kwanza. Pili ni kwamba kufikia Januari nitakuwa nimepata fursa ya kufanya mazoezi na kikosi changu chote. Kwenye mechi hizo tano, tumekuwa hatuna kikosi chetu mahususi,” alijichocha kocha huyo raia wa Ubelgiji.
Kauli ya Aussems inarejelea wachezaji 10 waliosajiliwa kabla ya msimu kuanza ila Ingwe ikashindwa kuwatumia kutokana na wao kukosa kuidhinishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Ingwe iliwasiliji 10 hao ligi ilipokuwa ikisimamiwa na Kamati Shikilizi, isiyotambuliwa na FIFA, kabla ya ofisi ya FKF kurejeshwa uongozini. Ingwe inahudumia marufuku ya kutosajili kufuatia tendo la kukiuka maagizo ya FIFA ya kuwafidia wachezaji wao wa zamani.
Hata hivyo kati ya 10 hao, wanne waliidhinishwa na FIFA wiki iliyopita baada ya Ingwe kumaliza kulipa fidia ya wachezaji wanne iliyowavunjia mikataba pasi na kuzingatia utaratibu. Sasa wamesalia sita ambao kocha Aussems anasema ana uhakika kufikia Janauri nao watakuwa wameidhinishwa.
Kando na Ingwe kuwa na kikosi hafifu, timu imeonyesha kushindwa kupachika mabao ya kutosha ambapo kwenye mechi hizo tano, Ingwe wana mabao matatu tu.
“Hiyo ni ishu kubwa ila limetokana na ukosefu wa wachezaji wetu wazoefu ambao wengi wao hatujaweza kuwatumia hadi hivi majuzi kutokana na kutoidhinishwa kwao na FIFA. Ila kuanzia Janauri nina uhakika mambo yatabadilika,” alisema Aussems.