Aussems apiga sherehe

KOCHA mkuu wa AFC Leopards, Mbelgiji Patrick Aussems, bado hajarejea nchini ikiwa ni siku nne tangu Ingwe walipoamza mazoezi yao ya maandalizi ya msimu mpya 2022/23.

Imesalia mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya na ndio sababu Ingwe iliingia kambini angalau kuanza kuandaa utitamu wa mwili wa wachezaji wake kabla ya shughuli nzima kuanza.

Walianza kambi ya mazoezi yao Jumatano kwa kuingia gym na kula vyuma kisiwa sawa, mchakato ambao wamekuwa wakiuchanganya na mazoezi ya uwanjani kwa siku chache zilizopita sasa.

“Timu iliingia kambini Jumatano kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya. Kikao chetu cha kwanza kilikuwa kwenye gym kisha siku iliyofuata tukaingia uwanjani kuanza kuzipasha misuli moto,” alifafanua Katibu Mkuu wa Ingwe, Gilbert Andugu.

Hata hivyo uongozi wa Ingwe unasema hauna hofu ya kuanza mazoezi pasi na uwepo wa kocha wao wanaoamini atarejea.

Uongozi huo unasema bado Aussems ana siku zingine 15 zaidi za kupiga sheria kabla ya kufunga safari ya kurejea Kenya kuendelea na majukumu yake.

Kumekuwepo na tetesi kibao zinazomhusisha Aussems na kuhamia klabu nyingine hususan za Rwanda huku Kiyovu SC ikihusishwa naye.

“Tumeshafanya kikao cha zoom na kocha wetu ambaye bado anaendelea na likizo yake kule Ubelgiji na tunamtarajia nchini kufikia Agosti 12. Alituhakikisha na kutukatia kauli kabisa kwamba atafika tarehe hiyo na tunamwamini,” ameongeza Andugu.

Aussems aliondoka nchini ligi kuu ikiwa imesalia na mechi mbili kufika mwisho huku mkataba wake na Ingwe ukitarajiwa kufika kikomo mwishoni mwa mwaka huu.