AMINA ALIVYOMFICHIA GAME MWENDWA NA KUITEKA KANDANDA HOUSE

KUVUNJWA kwa afisi ya Shirikisho la soka nchini FKF iliyokuwa ikiongozwa na Nick Mwendwa, na serikali ulikuwa ni mpango  ulioanza kufanyiwa utarataibu muda mrefu.
Wizara ya michezo chini ya Waziri Balozi Amina Mohammed, ilifahamu fika kuwa hatua ya kumtengeua Mwendwa na afisi yake nzima iliyochaguliwa tena 2020, itaibua hisia kali na hata tishio la kufungiwa na FIFA.
Hesabu zote hizi zilifanywa na Wizara kabla ya Amina kufanya uamuzi huo wa kumtengua Mwendwa akiwa Uganda juzi Alhamisi. Afisi yake ikakabidhiwa kamati huru ya wanachama 15 inayoongozwa na jaji mstaafu Aaron Ringera, na kitengo spesheli Secretrait ya wanachama 12 inayoongozwa na mtangazaji wa habari runingani Linda Oguttu.
Vitengo hivi viwili, vitaendesha shughuli za soka nchini kwa miezi sita katika kipindi ambacho uchaguzi mkuu unapaswa kufanywa ili kuchagua viongozi wapya.
Kulingana na taarifa za utendeti, Wizara ilikuwa imechoshwa na ubadhirifu wa fedha za serikali zilizotolewa kwa FKF. Wizara inamshutumu Mwendwa na Afisa Habari wake Barry Otieno kuwa wabadhirifu wakubwa wa fedha hizo zilizonuwiwa kuimarisha soka nchini.
Amina alichukua uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya mapendekezo kutoka kwa kamati ya Uchunguzi iliyobuniwa kufanya ukaguzi kwenye madaftari ya FKF. Ripoti hiyo ilipendekeza uongozi wa sasa uondolewe na kamati shikilizi ibuniwe kuendesha soka kwa muda wa miezi sita.
Akitetea uamuzi wake, Amina alisema kuwa uamuzi kama huo umefanikiwa katika mataifa mengine ikiwemo Cameroon, Misri, Ghana na Chad katka jitihada za kurejesha soka kwenye mustari
Mara tu baada ya kutenguliwa, maafisa wa usalama walitumwa kwenye makao makuu ya FKF, Kandanda House, makao yaliyoundwa na fedha za serikali.


Mwendwa ambaye anasisitiza kuwa bado ndiye anayeongoza soka la Kenya, amedhibitisha kuzuiliwa kuingia Kandanda House yeye na wafanyikazi wake.
"Uamuzi huu ni kinyume na sheria. Sioni nilikokosea mimi. Kamati hii hatuitambui. Hatujapatikana na hatia yeyote. Tumewafahamisha FIFA tayari na wametoa mwongozo wao. Mwanachama yeyote wa soka asisikize maelekezo ya Kamati hiyo. Bado tupo madarakani na sisi ndio tutasimamia mechi dhidi ya Rwanda Jumatatu."Mwendwa kasema baada ya kurejea nchini.
Mchakato wa Amina na Wizara yake ulianza zaidi ya miezi miwili iliyopita. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kumwandikia barua Rais wa FIFA Gianni Infantino kumfahamisha kuhusu madai ya uongozi mbaya wa FKF yaliyokuwa yakiathiri timu ya taifa. Kisha baada ya barua hiyo, Amina aliiamua msajili wa Michezo  (Sports Registrar) kufanya upekuzi wa vitabu vya uhasibu vya FKF.
Akiwahutubia wanahabari, Amina amesema kila alipochukua hatua na uamuzi, alihakikisha anawafahamisha FIFA.