Yatakayojiri Simba Day

SIMBA Day itakayofanyika leo Jumatatu itakuwa ya 14 tangu ilipoanzishwa mwaka 2009 na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali anaeeleza malengo ya tamasha hilo.

Dalali aliyesaidiana wazo hilo na aliyekuwa katibu wake, Mwina Kaduguda anasema kupitia tamasha hilo walihitaji kupata pesa ya kununua na kujenga Uwanja wa Bunju, kutambulisha kikosi chao cha msimu, mashabiki kutoa baraka kwa mastaa wao na kurudisha shukrani kwa jamii.

“Ninajisikia faraja kwa sababu ni wazo linaloishi na limekuwa na manufaa makubwa, viongozi wamejitahidi kuongeza ubunifu mkubwa unaofanya klabu inufaike nalo,” alisema.

Mwanaspoti linakuchambulia yatakayojiri katika tamasha hilo na tayari hamasa zimeanza kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally akiyataka matawi kufanya mambo ya kijamii katika maeneo yao.

Jambo alilolisisitiza Ahmed ni kuona Simba Day ya mwaka huu inakuwa ya kihistoria: “Kwanza nayaomba matawi yafanye amsha amsha kabla ya kilele cha siku yenyewe, kuhakikisha inaandikwa historia ya kusimuliwa.”

SAPRAIZI YA KIKOSI

Bado mashabiki wa Simba wana sintofahamu kuhusiana na kikosi kitakachowawakilisha kwenye Ligi Kuu msimu ujao, hivyo kupitia tamasha hilo watajua nani kaingia na nani ametoka.

Huenda kutakuwa na spraizi kwenye tamasha hilo kutokana na namna ambavyo Simba imejiandaa na kauli mbiu yao ya ‘Unstoppable’

Huenda pia itatumia nafasi hiyo kuwaaga nyota wake watatu iliuyowatema Meddie Kagere aliyewahi kuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo na ameishatua Singida Big Stars alikotambulishwa tayari kwenye tamasha lao, Tadeo Lwanga aliyetua Vipers ya kwao Uganda na Chris Mugalu.


AHMED ATAKUWA NA JIPYA GANI

Tangu Simba imwajiri Ahmed alipokewa kwa mikono miwili na mashabiki wa timu hiyo, lakini bado unasubiriwa ubunifu wake wa nini atakifanya katika tamasha hilo.

Ahmed anajua kucheza na mitandao ya kijamii na kuandika vitu vinavyowapa raha mashabiki wa Simba ni kama amefiti nafasi ya aliyekuwa msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara anayeitumikia Yanga kwa sasa.


TUZO YA SAKHO

Kama kuna kitu kimewafariji mashabiki wa Simba ni Tuzo ya Bao Bora la Afrisha mwaka 2022 aliyoipata winga wao, Ousmane Sakho, jambo lililoonekana kuwachangamsha mashabiki na iliwarejesha kufanya utani kwenye mitandao ya kijamii.

Katika tamasha hilo, Sakho atashangiliwa zaidi kutokana na mafanikio aliyopata na huenda akaipeleka tuzo hiyo uwanjani.


JE, NI MPOKI TENA ?

Wakati Simba inauanza msimu wa 2021/22 msanii wa vichekesho nchini, Silvery Mjuni ‘Mpoki’ ndiye aliyenogesha utambulisho wa wachezaji akisaidiana na Mkongwe wa Hip Hop, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ walifanikiwa kulinogesha tamasha hilo. takuwa sapraizi kwa mashabiki wa Simba kama atakayewatambulishia mastaa wao atakua Mpoki ama mtu mwingine.


MASTAA WATAKAONG’ARA

Katika utambulisho huo, lazima kutakuwepo na mastaa ambao nyota zao zitang’ara, tayari baadhi yao majina yamepata umarufu kabla ya kukutana na mashabiki wao.

Mastaa hao watakutana na mashabiki wao kwa mara ya kwanza Kati ya hao yupo Augustine Okrah kutoka (Bechem United), Mohammed Ouattara (Al Hilal), na Moses Phiri kutoka Zambia. Wengine ni Nelson Okwa wa Nigeria, Victor Akpan Mnigeria aliyesajiliwa akitokea Coastal Union, Nassoro Kapama kutoka Kagera Sugar, Habibu Kyombo (Mbeya Kwanza).