Yanga yavamia Simba, yampandia ndege straika matata

SIMBA ipo Kisiwani Zanzibar huku mabosi wao wakiendelea na hesabu za kukisuka kikosi chao lakini habari mbaya ikawafikia na kuwashtua kuwa mmoja wa mastraika waliokuwa wawasajili amebakiza hatua chache kutua kwa watani wao Yanga.

Iko hivi Simba imepata taarifa za uhakika kutoka Zambia kwamba bosi wa usajili ndani ya Yanga Mhandisi Hersi Said yupo nchini humo tangu jana akifanikisha mipango ya kumchukua straika Mosses Phiri.

Phiri ambaye anaitumikia Zanaco ya Zambia Simba ilikuwa inapiga hesabu za muda mrefu za kumchukua katika mpango wa kuifanyia kazi ripoti ya kocha wao Pablo Franco ambaye anahitaji straika mwenye kasi.

Ghafla Hersi akaonekana nchini Zambia kisha taarifa hizo zikawafikia Simba ambao wakajikuta wanachanganyikiwa na hatua hiyo wakiomba Mungu pande hizo mbili zishindwe kukubaliana.

Hatua mbaya zaidi katika uwepo wa Hersi nchini Zambia ni kwamba wakala wa Phiri ameshindwa kupokea simu za mabosi wa Simba hatua ambayo imezidi kuleta wasiwasi wa usalama wa mshambuliaji huyo.

Hata hivyo, Zanaco ndio waliokuwa wanaweka ugumu katika kuuzwa kwa Phiri ambaye anaweza kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati na hata kutokea pembeni, wakitaka mshambuliaji huyo kusalia katika kikosi chao wakidai kama ataondoka watakuwa wameibomoa timu yao.

“Tulisikia tangu juzi lakini leo (jana)tumepata uhakika kwamba Hersi ni kweli yuko nchini Zambia na amemfuata Phiri, lakini acha tuone kama watakuwa wamemalizana,” alisema bosi huyo ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya klabu hiyo.

“Ni kama (Yanga) wameamua kutaka kutuharibia hesabu zetu ila hatutakata tamaa tunaendelea kufuatilia hili na wakifanya makosa tutamaliza biashara.”

Yanga inatafuta straika atakayeweza kutokea kushoto kuziba nafasi ya Yacouba Songne ambaye alifanyiwa upasuaji wa goti na sasa ameanza kufanya mazoezi mepesi akihitajiwa na kocha wa timu hiyo Nesreddine Nabi.

Phiri ambaye kwasasa Zanaco imekuwa ikimtumia kama mshambuliaji wa kati anatisha pia anapocheza akitokea pembeni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuwapunguza mabeki, kufunga na kutoa asisti za mabao kwa wachezaji wenzake.