Yanga yatua Dar, yaingia kambini kujifua kuivaa Geita

Muktasari:

BAADA ya klabu ya Yanga kuwasili jijini Dar es Salaam leo mchana wakitokea mkoani Kagera walipokuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar wameelekea moja kwa moja kambini kwao Avic Town Kigamboni.

BAADA ya klabu ya Yanga kuwasili jijini Dar es Salaam leo mchana wakitokea mkoani Kagera walipokuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar wameelekea moja kwa moja kambini kwao Avic Town Kigamboni.

Baada ya kikosi hicho kutua, wachezaji walielekea kambini moja kwa moja kujiandaa na mchezo utakaopigwa Jumamosi hii dhidi ya Geita Gold, utakaochezwa katika dimba la Mkapa saa moja usiku.

Ikumbukwe kuwa baada ya kikosi cha Yanga kupata ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Kagera Sugar, kikosi hicho kitakuwa na mtihani wa kuhakikisha kinavuna pointi tatu nyingine kwa ajili ya kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi mara baada ya kuwasili anasema walikuwa na mechi nzuri kwa maana ya kupata pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar ugenini.

Nabi anasema katika kucheza kama ambavyo walihitaji hawakuwa katika kiwango bora kutokana na changamoto mbalimbali ambazo walikutana nazo.

Anasema hakuna mapumziko kwa wachezaji wake kwani wanahitaji kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi ambao nao wamepungua kupata pointi na kucheza vizuri.

“Bado tupo kupambana na kutengeneza kikosi chetu kuwa imara zaidi katika mashindano haya ya ndani na kufikia mafanikio,” anasema Nabi na kuongeza;

“Imani yangu kubwa tutazidi kuimarika kuwa na matokeo mazuri pamoja na mchezo mzuri katika siku zijazo kutokana na kuendelea kukaa pamoja.”