Yanga yatoa msimamo kifungo cha Mwakalebela

Tuesday April 06 2021
yanga pic mwakalebela
By Imani Makongoro

Klabu ya Yanga imetoa msimamo juu ya adhabu aliyopewa makamu mwenyekiti wao, Fredrick Mwakalebela ikisisitiza kukata rufaa kuipinga.

Kamati ya maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivi karibuni ilimfungia kwa miaka mitano kutojihusisha na soka na kutakiwa kulipa faini ya Sh7 Milioni kigogo huyo akimshutumu kwa makosa ya kimaadili.

Mwakalebela alilalamikiwa kuzungumza na vyombo vya habari Februari 19 na kudai TFF, Bodi ya Ligi na Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi zinaihujumu Yanga, madai ambayo alishindwa kuyathibitisha mbele ya kamati.

Pia shitaka jingine kwa kiongozi huyo wa Yanga ni la Oktoba Mosi mwaka jana kudai kuwa na mkataba wa Bernard Morrison na klabu ya Simba huku akijua ni uongo.

Akizungumzia adhabu hizo, ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kama klabu inaipinga na iko mbioni kukata rufaa.

"Tumechelewa kukata rufaa kwa kuwa tulikuwa tunasubiri muongozo wa TFF, lakini kama klabu hatujakubaliana na adhabu hiyo kwa makamu mwenyekiti wetu," amesema Bumbuli.

Advertisement

Amedai klabu imeshangazwa na suala hilo kuwa la binafsi na kufungiwa Mwakalebela wakati kilichopelekea afungiwe ilikuwa ni uamuzi wa klabu na si wa Mwakalebela.

"Mwakalebela alizungumza kile kilichoamuliwa na klabu, na hadi anakizungumza ilikuwa ni uamuzi wa klabu, lakini ameadhibiwa kama Mwakalebela.

"Klabu hatujakubaliana na adhabu hiyo na wakati wowote kuanzia sasa tutawasilisha rufaa kupinga adhabu aliyopewa makamu mwenyekiti wa klabu yetu," amesema Bumbuli.

Akizungumzia taarifa inayotembea kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha klabu hiyo imeomba kufanya maandamano ya amani, Bumbuli alisema si kweli ni taarifa za uongo.

Advertisement