Yanga yamtuliza Tambwe kiaina

STRAIKA wa zamani wa Yanga, Amissi Tambwe ameendelea kuikalia kooni klabu hiyo akisema bado haijamalizana naye lakini uongozi huo ukamjibu na kumtuliza.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa alikiri ni kweli bado hawajamalizana na Tambwe na wala hawana wasiwasi wa kufikia hatua ya kufungiwa.

Mfikirwa akifafanua zaidi alisema wanachofanya sasa ni kuweka sawa kumbukumbu ya deni hilo wakishirikiana na uongozi wa mchezaji huyo ili waweze kumalizana.

“Hukumu ile inasema mpaka tukifika wakati wa dirisha la usajili tukiwa bado hatujalipa ndio hukumu ya kifungo itatekelezwa lakini hebu angalia ni muda gani hapa umesalia kufikia huko.”

Katibu huyo aliongeza; “Niseme kwamba kama klabu hatutasubiri kufika wakati huo tutakuwa tayari tumeshamaliza hii kesi isipokuwa sasa tunachofanya ni kuweka sawa kumbukumbu za deni hilo ili klabu iweze kumaliza hili suala. “Hatupendi kuwa tunasema sana lakini tunachofahamu Tambwe ana watu ambao wanamsimamia kesi hii tunaendelea kushirikiana nao na tutamalizana naye ndani ya wakati.”