Yanga yamrudisha Makambo

Muktasari:

MASHABIKI wa Yanga hawafurahii ushindi mwembamba wa timu yao, lakini staa wao mmoja ametaja sababu ya hali hiyo, huku wengine wawili wakituma jina moja kwa mabosi wao kwamba Heritier Makambo kama vipi arudishwe tu Jangwani.

MASHABIKI wa Yanga hawafurahii ushindi mwembamba wa timu yao, lakini staa wao mmoja ametaja sababu ya hali hiyo, huku wengine wawili wakituma jina moja kwa mabosi wao kwamba Heritier Makambo kama vipi arudishwe tu Jangwani.

Kipa namba mbili wa Yanga, Farouk Shikhalo ameiambia Mwanaspoti kuna staa mmoja tu amesalia kunogesha soka la Kocha wao Cedric Kaze na kama itafaa basi mabosi wao wamrudishe Makambo ambaye hana shaka naye katika kazi ya kufunga.

Tangu aondoke Makambo kujiunga na AC Horoya ya Guinea, Yanga imekuwa ikihaha kusaka kupata straika wa kutupia mwenye ufundi kama Mcongo huyo ama Amissi Tambwe na msimu uliopita walikuwa na David Molinga na kuwaleta Juma Balinya, Sadney Urikhob waliochemsha.

Msimu huu ikiwa na Michael Sarpong, Yacouba Songne, Wazir Junior na Ditram Nchimbi Yanga imefunga mabao 15 katika tu mechi 13 ikiwa ni wastani wa bao moja kila mchezo kitu ambacho kinawakera mashabiki wao wanaokejeliwa na wenzao wa Simba inayotupia sana nyavuni ikifunga mabao 29 katika mechi 11 tu.

Shikhalo alisema, anamfahamu Makambo na ubora wake katika kufunga, kujua kujipanga ndani ya eneo la hatari na kwamba kama jamaa atarejea basi vicheko vitatawala.

Kipa huyo raia wa Kenya alisema Makambo ni mshambuliaji aliyekamilika na kwamba kwa kikosi chao atakuwa na kazi rahisi ya kufunga atakavyo.

“Tuna shida ya kutumia nafasi na ukishakuwa unapoteza nafasi lazima utajiweka katika mazingira magumu, mi naona tunahitaji mtu wa kufunga kwa nafasi tunazopata na ukiniuliza mimi aje nani nitakutajia Makambo,” alisema Shikhalo.

“Yule ni mshambuliaji aliyezaliwa kwa kazi ya kufunga, anajua kujipanga na kufunga. Kwa timu yetu ninavyoiona tutakuwa tumeleta mtu atakayerudisha uhakika wa safari yetu ya ubingwa.”

Mbali na Shikhalo, beki wa kulia Paul Godfrey ‘Boxer’ ni kama amekazia hapo kwa Makambo akisema anatamani ujio wa mshambuliaji huyo Mkongomani katika timu yao.

Boxer ambaye alianza kwa mara ya kwanza katika mechi ya ligi juzi dhidi ya JKT Tanzania alisema kwa krosi zinazopigwa sasa katika kikosi chao na hata nafasi haziwezi kupotea bure kwa Makambo.

“Tunapiga krosi nyingi sana sasa, lakini kuna nafasi nyingine zinahitaji umakini mdogo tu kumalizia. Vitu kama hivyo Makambo hawezi kukuacha. Kama akirudishwa itakuwa ni hatua kubwa,” alisema Boxer, aliyecheza na Makambo misimu miwili iliyopita.

Mpaka anaondoka Jangwani kwenda AC Horoya ya Guinea, Makambo alifunga mabao 17 akiwa ndiye kinara wa mabao wa Yanga nyuma ya Meddie Kagere wa Simba aliyemaliza Mfungaji Bora.


MSIKIE MUKOKO

Kiungo Mukoko Tonombe amefunguka kwamba mashabiki wasiwe na hasira sana na timu yao kutokana na wao kukumbana na uchovu baada ya kucheza mechi nyingi ndani ya siku chache.

Tonombe alisema asilimia kubwa ya wao waliathirika na uchovu ambapo wamecheza mechi tatu ndani ya siku nane tena zikiwa mechi ngumu.