Yanga yaizamisha Mtibwa

Saturday February 20 2021
New Content Item (1)
By Thobias Sebastian
By Olipa Assa

FURAHA imerejea tena Jangwani, baada ya nyota wao kutoka Angola, Carlinhos kufunga bao pekee lililowazamisha Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika kipindi cha kwanza mchezo huo ulimalizika bila mabao licha ya kosa kosa nyingi kwenye muilango ya timu zote.

Katika mechi hiyo Yanga walianza kwa kasi ya kupeleka mashambulizi aina tofauti katika lango la Mtibwa na yote yalipotea kwa kuokolewa na mengine kutoka nje.Yanga ndani ya dakika 10, za mwanzo walifanya mashambulizi ya mara kwa mara kupitia kwa winga wake wa kulia, Ditram Nchimbi ambaye kuna wakati alifanikiwa kumpita beki wa kushoto wa Mtibwa, Issa Rashid na kuleta hatari ila muda mwingine alishindwa.

Advertisement

Mashambulizi mengine ya Yanga yalikuwa yakipita kwa Tuisila Kisinda kutokana na kasi yake alimzidi, Hassan Kessy aliyekuwa akimkaba na kupiga krosi nyingi ambazo hazikuzaa mabao.

Dakika 36, shuti kali la Feisal Salum ambalo lilimgonga beki wa Mtibwa na likiwa linaelekea langoni kipa, Abuutwalib Mshery alilipangua na kuwa kona.

Ukiondoa shambulizi hilo la Feisal, Yanga hawakufanya lingine lenye hatari zaidi huku, Michael Sarpong na Deus Kaseke walikuwa wakipoteza mipira mara kwa mara.

Wakati Yanga wakiingia na plani ya kushambulia zaidi ambayo haikufanikiwa kuzaa bao katika kipindi cha kwanza, Mtibwa wao walikuwa na malengo yao tofauti.

Mtibwa walikuwa na nidhamu kubwa katika ulinzi na muda mwingi walifanikiwa kuwazuia washambuliaji wa Yanga licha ya muda mwingine kufanya makosa.

Mtibwa walikuwa wakicheza soka la kupasiana pasi fupi fupi na muda mwingine kushambulia kwa kushtukiza kutokana na kumsimamia, Kelvin Sabato mwenyewe katika eneo lao la kushambulia.

Dakika 45, Mtibwa Sugar walifanya shambulizi la hatari kupitia kwa Issa Rashid ambaye alipiga shuti kali la juu lililokuwa likielekea langoni ila Farouk Shikhalo alilipangua.

Mtibwa licha ya kukosa shambulizi hilo, viungo wao wawili Barako Majoro aliyecheza nafasi ya ukabaji na Kassim Hamis walikuwa wakicheza vizuri na kuwapata wakati mgumu viungo wa Yanga.

Katika kipindi cha pili, Yanga waliendelea kushambulia mara kwa mara wakati Mtibwa wao walikuwa watulivu katika kukaba na kufanya mashambulizi mara chache ya kushtukiza.

Katika kuhakikisha wanaongeza makali katika safu yao ya ushambuliaji dakika 65, walifanya mabadiliko mawili walitoka, Kaseke na Sarpong na wakaingia, Fiston Abdulrazak na Farid Mussa.

Dakika 67, Mtibwa walimtoa Riphat Msuya aliyeumia na kutolewa nje kwa machela na nafasi yake aliingia, Haruna Chanongo, wakati Yanga dakika 71, alitoka Nchimbi na kuingia Carlos Carlinhos.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija kwa upande wa Yanga, walioendelea kushambulia zaidi ya hapo awali.

Ilimchukua dakika mbili tangu kuingia kwake, Carlinhos kwa kuifungia Yanga bao la kuongoza dakika 73, akiunganisha pasi safi ya chinichini kutoka kwa Kisinda.

Mtibwa baada ya kufungwa bao hilo walibafilisha aina yao ya uchezaji wa kujilinda zaidi na kuanza kushambulia moja kwa moja.

Yanga baada ya kupata bao hilo walibadili aina yao ya uchezaji na kucheza kwa kujilinda zaidi huku Mtibwa wakifanya mashambulizi ambayo hayakufanikiwa kuzaa bao.

Mpaka dakika 90, zinamalizika Yanga walifanikiwa kupata pointi tatu baada ya ushindi huo wa bao 1-0, ambalo lilifungwa na Carlinhos aliyeingia kipindi cha pili.

Advertisement