Yanga ‘yaitimua’ Ruvu Shooting Dar

BAADA ya kuchezea kichapo jana cha bao 1-0, dhidi ya Yanga, Ruvu Shooting imeamua kukimbilia uwanja mpya wa Jamhuri mkoani Morogoro ambao itautumia kwa mechi zake za nyumbani zilizobaki.

Ruvu Shooting haijawa na matokeo mazuri kwenye ligi kuu ikiwa mkiani kwa sasa kwa pointi 14 baada ya kucheza michezo 21 ikibakiza tisa pekee.

Kwa muda mrefu timu hiyo ilikuwa ikitumia uwanja wa Mabatini mkoani Pwani kabla ya kufungiwa na kuhamishia mechi zake uwanja wa Uhuru na Mkapa na sasa inatimka Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Maafande hao katika mechi tisa zilizobaki kumaliza msimu, itacheza nne nyumbani ikianza KMC, Kagera Sugar, Azam na Dodoma Jiji huku tano ikicheza ugenini dhidi ya Geita Gold, Mbeya City, Prisons, SBS na Simba.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata amethibitisha mabadiliko hayo akisema ni suala la kawaida na kwamba anaamini watafanya vizuri.

“Ni sahihi tumehamia Jamhuri Morogoro ni kawaida ya mabadiliko na timu itakuwa huko kwa mechi za nyumbani tunafahamu ugumu na umuhimu wake lakini matarajio ni kufanya vizuri,” amesema Makata.