Yanga yaichapa Mwadui dakika za mwisho

Sunday June 20 2021
full pic
By Ramadhan Elias

Mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Mwadui umemalizika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji Yanga kutoa kichapo cha bao 3-2.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote mbili kufungana bao 1-1, Mwadui wakitangulia kufunga dakika ya saba kupitia kwa Aniceth Revocatus kabla ya Yanga kusawazisha dakika ya 21 kupitia kwa Bakari Mwamnyeto.

Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi ya kawaida na dakika  ya 55 Mwadui walifanya mabadiliko kwa kumtoa Makyada Makolo na nafasi yake kuchukuliwa na Denis Richard.

Tuisila Kisinda wa Yanga dakika ya 59 aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Zawadi Mauya aliyekuwa akicheza eneo la kiungo mkabaji sambamba na Mukoko Tunombe.

Dakika ya 65 yule yule Aniceth aliyeifungia Mwadui bao la kwanza alipachika bao la pili kwa timu hiyo kwa kupiga shuti kali nje ya boksi la Yanga na kuzama nyavuni moja kwa moja likimshinda kipa wa Yanga Farouk Shikhalo.

Yanga ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 68 Yanga ilimtoa Fiston AbdulRazack aliyeonekana kukosa nafasi nyingi za wazi na kuingia Yacouba Sogne.

Advertisement

Dakika ya 75 Mwadui walifanya mabadiliko kwa kumtoa Richars aliyeingia kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Amri Msenda huku Yanga nao dakika ya 80 wakimtoa Said Ntibazonkiza na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Junior.

Dakika ya 90, Yacouba aliisawazishia Yanga baada ya kulishambulia lango la Yanga mfululizo kwa dakika zisizopungua tano na sekunde chache baadae Junior aliwafingia Yanga bao la tatu na la ushindi katika mechi hiyo.

Ushindi huo umeifanya Yanga kujikita katika jafadi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha alama  67 baada ya mechi 31.

Advertisement