Yanga yaichapa Mbeya City ikiandika rekodi mpya

MATOKEO ya leo Yanga ikiichapa Mbeya City mabao 2-0 inafikisha mechi 49 bila kupoteza mchezo wowote kwenye ligi pia inazidi kujiimarisha kukaa kileleni, ikifikisha pointi 32, katika mechi 12 iliyozocheza.
Ukiachana na kichapo cha leo ilichopata Mbeya City, mara ya mwisho kuifunga Yanga ilikuwa Novemba 2, 2016 Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Wakati matokeo ya misimu miwili iliyopita, Mbeya City 1-1 Yanga (Juni 25,2021/ 22),Yanga 0-0 Mbeya City (Februari 5,2021/22),Yanga 1-0 Mbeya City (Septemba 13, 2020/21),Mbeya City 1-1 Yanga (Februari 13, 2020/21).

Hata hivyo matokeo hayo kwa Mbeya City, yataifanya kushuka nafasi za chini, kwani katika mechi 13 ilizocheza imeshinda nne, sare sita, imefungwa mitatu inamiliki mabao 18 imetikiswa mara 16 na pointi 18.

Mayele amefunga mabao saba katika michezo mitatu ya ligi akianza na hat-trick dhidi ya Singida BS, mawili dhidi ya Dodoma Jijj na leo dhidi ya Mbeya City.

Kinara huyo amefikisha mabao 10 akifuatiwa na Sixtus Sabilo-7, Moses Phiri, Reliant Lusajo-6.

Kipindi cha kwanza mabeki wa Mbeya City, walikuwa wanaacha mwanya ambao Fiston Mayele aliutumia vyema dakika ya 24 kuzitikisa nyavu zao baada ya kupokea pasi ya Khalid Aucho.

Ingawa kipindi cha pili, City ilijitahidi kumiliki mpira, ila ilikosa mipango ya kufika golini kwa Yanga, hivyo wakakuta wanaongezwa bao la pili, akifunga Mayele dakika ya 79 akipokea pasi ya Jesus Moloko.

Katika mchezo huo, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko ya kuwatoa  Gael Bigirimana /Aziz Ki, Tuisila Kisinda/ Denes Nkane, Mayele/ Clement, Aucho/Mauya.