Yanga yabakiza sita tu za ubingwa

Yanga yabakiza sita tu za ubingwa

YANGA imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufanya kubakiza alama sita pekee ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 63 baada ya mechi 25 za Ligi huku ikihitaji alama sita kwenye mechi tano zilizobaki ili kuwa bingwa kwani itafikisha jumla ya pointi 69 ambazo hakuna timu yeyote itazifikisha baada ya mechi zote kumalizika.

Pia ushindi  huo umeifanya Yanga kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi kwenye Ligi msimu huu ikiwa imecheza 25 kushinda 19 na sare sita.

Wakati Yanga ikichekelea na ushindi huo, hali si shwari kwa Mbeya Kwanza kwani imeendelea kusalia mkiani mwa msimamo wa Ligi na alama zake 21 ikiwa imebaki na mechi tano tu.


MCHEZO ULIVYOKUWA
Kipindi cha kwanza kilimaliza Yanga ikiongoza kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Fiston Mayele dakika ya 33, Said Ntibanzokiza ‘Saido’ 37 na Dickson Ambundo dakika ya 45.

Kipindi cha pili kilirejea kwa timu zote kutafuta mabao, Yanga ikimiliki mpira kuanzia dakika ya 45 hadi 48 kisha Mbeya Kwanza kupokonya mpira na kushambulia.
 
Kuanzia dakika ya 48 hadi 55 Mbeya Kwanza ilikiwa eneo la Yanga ikitengeneza nafasi za kupata bao zaidi ya mara tatu lakini wachezaji wake walikosa utulivu na kukosa mabao.

Licha ya wachezaji wa Mbeya Kwanza kukosa utulivu lakini Yanga itajivunia ubora wa kipa wake Djigui Diarra kwa kuokoa michomo mitatu ya hatari katika muda huo.

Dakika ya 59 Yanga ilifanya mabadiliko manne kwa wakati mmoja wakiingia Zawadi Mauya, Heritier Makambo, Crispin Ngushi na Chico Ushindi kuchukua nafasi za Ambundo, Sureboy, Jesus Moloko na Mayele.

Dakika ya 60 Mbeya kwanza ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Fredrick Mgata na kuingia Mohamed Kapeta na baadae kidogo alitoka Farid Mussa kwa upande wa Yanga na kuingia Mustapha Yassin.

Dakika ya 73 Yanga ilipata bao la nne kupitia kwa Makambo likiwa bao lake la kwanza kwenye ligi msimu huu akiunganisha kwa kichwa pasi ya Ushindi.

Kuingia kwa Makambo na Ushindi kuliongezea Yanga nguvu eneo la ushambuliaji na kutengeneza nafasi zaidi za kufunga lakini walishindwa kuzitumia vyema.

Hadi dakika 90 zinamalizika, Yanga 4-0 Mbeya Kwaza.