Yanga yaanza na sare Kagame, yatambulisha wapya

MECHI ya ufunguzi ya mashindano ya Kombe la Kagame 2021 kati ya Yanga ya Tanzania na Nyasa Big Bullets ya Malawi imemalizika kwa sare ya bao 1-1, huku Yanga ikitambulisha baadhi ya wachezaji wake iliyowasijili kwa msimu ujao.

Ikiwa na Razak Siwa kama Kocha Mkuu kwenye mashindano hayo, Yanga iliwachezesha nyota wake hao akiwamo Dickson Ambundo na Jimmy Julio Ukonde kutoka Msumbiji, huku Fiston Mayele naye akishuhudia akiwa jukwaani.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa sare ya bao 1-1, mabao yaliyofungwa na Waziri Junior kwa upande wa Yanga akifunga dakika ya 8, kabla ya  Chiukepo Msowoya kuisawazishia Nyasa dakika ya 29 kwa mkwaju wa penati baada ya Abdalah Shaibu ‘Ninja’ wa Yanga kumchezea rafu Babatunde Adepoju wa Nyasa.

Kipindi kilirejea kwa timu zote mbili kuanza kwa kasi kila moja ikitafuta bao la kuongoza lakini hadi dakika ya 75 hakuna aliyekuwa amepata bao.

Eneo la kiungo lilionekana kuwa na ushindani na ufundi mkubwa zaidi katika mechi ya leo ambapo viungo Chibada Kabago na Best Kahemela wa Yanga walionekana kupata changamoto kutoka ka stiven Munthali na Macfallen Mgwira wa Nyasa.

Dakika ta 83 Paulo Godfrey wa Yanga alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Nyasa, Hassan Kajoke nje kidogo ya eneo la boksi la Yanga.

Baada ya hapo nyasa walipiga pigo la faulo na mpira kupaa juu lakini dakika moja baadae Nyasa kupitia kwa Kajoke alifanya shambulizi lililookolewa na kipa wa Yanga Ramadhan Kabwili.

Dakika ya 89 kipa wa Yanga, Kabwili alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea faulo ya makasudi mshambuliaji Kajoke wa Nyasa aliyekuwa akielekea langoni kwa Yanga.

Kadi nyekundu hiyo iliwalazimu Yanga kumfanya mabadiliko ya lazima kwa kumtoa mshambuliaji Julio Ukonde na nafasi yake kuchukuliwa na kipa Geofrey Magaigwa.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika Yanga 1-1 Nyasa Big Bullets.