Yanga ya ubingwa nomaa, Mayele atupia

Yanga ya ubingwa nomaa, Mayele atupia

Muktasari:

  • Mabao ya Mayele, Said Ntibanzokiza ‘Saido’ na Dickson Ambundo yametosha kuipeleka mapumziko Yanga ikiwa kifua mbele kwa mabao 3-0.

BAADA ya mechi nne mfululizo bila kufunga bao, nyota wa Yanga Fiston Mayele leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa amerejea kwenye makali yake akiifungia timu yake bao la kwanza dhidi ya Mbeya  Kwanza.

Mabao ya Mayele, Said Ntibanzokiza ‘Saido’ na Dickson Ambundo yametosha kuipeleka mapumziko Yanga ikiwa kifua mbele kwa mabao 3-0.

Yanga ndiyo imeongoza kwa kupeleka mashambulizi langoni kwa Mbeya Kwanza zaidi ya mara sita katika dakika 25 za kwanza lakini washambuliaji wake wakiongozwa na  Mayele walishindwa kutumia vyema nafasi hizo.

Eneo la kiungo la Yanga chini ya Khalid Aucho, Salum Abubakar ‘Sureboy’ na Saido sambamba na upande wa kulia walipocheza Farid Mussa na Dickson Ambundo ni maeneo yaliyokuwa bora kwenye kutengeneza mashambulizi.

Mbeya kwanza ilijikuta ikikaba zaidi kuliko kutengeneza mipango ya kushambulia na kupata bao kwani hadi dakika ya 20 hakuna shuti lililokuwa limelenga au kwenda nje ya lango la Yanga kwa kipa Djigui Diarra.

Katika kipindi cha kwanza nahodha wa Mbeya Kwanza, Salum Chuku alionyeshwa kadi ya njano dakika ya nane baada ya kumchezea madhambi Saido akiwa kwenye mwendo wa kasi.

Pamoja ja Yanga kutumia eneo la kati kati ya uwanja  na upande wao wa kushoto kushambulia, wachezaji wa Mbeya, Miza Kristom, Jimmy Shoji, Roland Msonjo na Chesco Mwasimba walikuwa bora kwenye kukaba.

Dakika ya 33 Yanga ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Mayele aliyefunga kwa kichwa akiunganisha pasi kutoka kwa Sureboy.

Bao hilo limekuwa la 13 kwa Mayele na kumfikia George Mpole wa Geita Gold kwenye mbio za kuwania ufungaji bora.

Ni kama bao hilo liliiamsha Yanga kwani dakika ya 37 ilifunga bao la pili kupitia kwa Saido aliyefunga kitaalamu kwa mguu wa kulia akipokea pasi safi ya Aucho.

Hilo ni bao la saba kwa Saido msimu huu kwenye ligi.

Hamis Kanduru na Brown Mwankemwa waliingia kwa upande wa Mbeya Kwanza kuchukua nafasi za Shoji na Chuku na dakika moja baadae Eliuter Mpepo alipika frikiki iliyookolewa na Diarra.

Dakika ya 45, Yanga ilipata bao la tatu kupitia kwa Ambundo aliyefunga kwa shuti kali baada ya kupokea na kutuliza pasi kutoka kwa Jesus Moloko na hadi dakika 45 zinamalizika, Yanga 3-0 Mbeya Kwanza.