Yanga wembe, Simba moto

MASHABIKI na wapenzi wa soka nchini leo wana kazi moja - kupata burudani wakati Simba na Yanga zitakapovaana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo mastraika wa timu hizo ndio wenye nafasi kubwa ya kuamua matokeo kwa vile wao ndio wachezaji wanaocheza karibu zaidi na lango la timu pinzani kuliko wengine.

Inawezekana wachezaji wa nafasi nyingine uwanjani wakafanya hivyo, lakini wanaotegemewa zaidi ni wale wa nafasi za ushambuliaji.

Ndio maana imekuwa sio jambo la kushangaza kuona wachezaji wa nafasi za ushambuliaji wakiwa na thamani kubwa katika soko la usajili kulinganisha na wale wa nafasi nyingine ingawa zipo nyakati mambo huwa tofauti.

Wakati vigogo hivyo vikikutana kwenye mechi yao ya nane kwenye Ngao ya Jamii tangu 2001, bado kuna matarajio makubwa kwa kila upande kwamba washambuliaji wao watakuwa chachu ya kupatikana kwa mabao yatakayoamua mchezo huo mkubwa wa kuzindua msimu mpya wa ligi.

Mwanaspoti linakuletea sifa za ubora wa washambuliaji ambao wana nafasi kubwa ya kucheza mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ambao kama wasipodhibitiwa vyema wanaweza kuacha kilio kwa timu mojawapo.


Fiston Mayele

Kasi, ujanja wa kuwatoroka mabeki, jicho la lango na uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa kichwa na kutumia miguu yote, vimemfanya awe mshambuliaji tishio katika siku za hivi karibuni hapa nchini.

Msimu uliopita alimaliza akishika nafasi ya pili kwenye chati ya wafungaji bora wa Ligi ya NBC akipachika mabao 16 lakini pia ndiye alifunga bao pekee la ushindi la Yanga dhidi ya Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii kama hii.


Heritier Makambo

Sifa yake kubwa ni uwezo wake wa kumiliki mpira mbele ya mabeki wa timu pinzani ambao wamekuwa wakipata wakati mgumu kumpora pindi unapokuwa miguuni mwake lakini pia amekuwa na maamuzi ya haraka mbele ya lango ambayo yamemfanya awe anafunga mabao hata kwenye mazingira magumu.


Lazarous Kambole

Ni mshambuliaji mwenye kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kufunga kwa kutumia mashuti ya mbali akiwa anatumia kwa ufasaha miguu yote miwili.


Bernard Morrison

Ni fundi wa kumiliki mpira, ana chenga za maudhi lakini pia akili yake inafanya kazi kwa haraka pindi mpira unapokuwa chini ya umiliki wake.

Morrison ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa kutumia mipira ya adhabu ndogo lakini pia ni mjanja wa kuwatoroka mabeki.


Aziz Ki Stephane

Ni hatari katika kupiga pasi za mwisho. Ana unyumbulifu na mikimbio ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu walinzi wa timu pinzani kumdhibiti.

Amekuwa akifunga mabao pindi anapopata nafasi akiwa jirani na lango la timu pinzani lakini pia uwezo wake wa kukokota mpira huwa mwiba kwa wapinzani.


Habib Kyombo

Amekuwa na maamuzi ya haraka pindi anapolisogelea lango la timu pinzani na hakati tamaa pindi anapokabiliana na walinzi wa timu pinzani.

Ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti na kunusa hatari pindi timu yake inaposhambulia.


Kibu Denis

Ni mshambuliaji ambaye amekuwa akitumia vyema umbile na nguvu zake kupambana na walinzi wa timu pinzani.

Amekuwa akifunga mara kwa mara kwa mashuti ya mbali na amekuwa na uwezo mkubwa wa kuficha mpira.


Clatous Chama

Fundi wa kukokota mpira, kupiga chenga za maudhi, kupiga pasi za mwisho na hata kufunga mabao pale anapopata nafasi mbele ya lango.

Akili yake hufanya kazi kwa haraka hasa katika kujua afanye nini pindi mpira unapokuwa miguuni.


Nelson Okwa

Kasi na uwezo wake wa kupiga chenga vimemfanya asiwe anapata wakati mgumu kuvunja ukuta wa timu pinzani na kutengeneza nafasi ama kufunga mabao.

Ni mchezaji mnyumbulifu na asiye na woga pindi anapokokota mpira kuelekea katika lango wanaloshambulia.