Yanga wamkosa Abraham, wasajili winga huyu

WINGA wa Biashara United, Yusuph Athuman mchana wa leo Agosti 2, ametambulishwa kuwa mchezaji mpya wa kikosi cha Yanga, ambacho kinaendelea kutangaza nyota wake wapya.

Baada ya kuhusishwa muda mrefu na kikosi hicho, hatimaye Athuman amejiunga na kikosi hicho kwa muda wa miaka mitatu.

Msimu ulioisha akiwa na kikosi cha Biashara, Athuman amecheza dakika 216 na kufunga mabao mawili aki asisti mbili hivyo kuhusika katika mabao manne.

Athuman alijiunga na Biashara United katika dirisha dogo la usajili akiwa mchezaji huru akitokea Namungo ambapo hakubahatika kucheza hata katika mechi moja ya kimashindano.

Yanga kabla ya kumsajili Athumani walikuwa wakimuhitaji Meshack Abraham kutokea Gwambina ambaye alishindwa kumalizana nao kutokana na kushindwa kukubaliana nao katika maslahi.

Athuman ambaye anacheza katika kikosi cha Yanga atakwenda kukutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa Tuisila Kisinda, Dickon Ambundo, Deus Kaseke, Ditram Nchimbi na Farid Mussa ambao wote wanacheza kwenye nafasi hiyo.