Yanga wamjibu Pablo, mastaa wakerwa na kauli yake

SIKU chache baada ya kocha mkuu wa Simba, Pablo Franco kutamka kuwa Yanga hawakustahili kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) wachezaji wa Yanga wamemtolea uvivu na kumtaka asubiri dakika 90 za mchezo huo ndio zitakazoamua nani alistahili.

Watani hao wa jadi wanatarajia kukutana Mei 28 mwaka huu kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza huku ukiwa ni mchezo wao wa pili kukutana hatua za mtoano awali ilikuwa ni nusu fainali Simba aliibuka na ushindi wa mabao 4-1 msimu wa 2020.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mastaa hao walisema hakuna mtu anazuiwa kuzungumza lolote analojisikia kuzungumza huku wakiweka wazi kuwa mpira hauchezwi mdomoni dakika 90 baina ya miamba 22 uwanjani ndio zinazoamua nani zaidi ya mwingine.

Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema wanaamini wao walistahili kwa mujibu wa matokeo waliyoyapata na kuwavusha kwenye hatua hiyo hawana maneno mengi zaidi ya utendaji na kumtaka Pablo wakutane Kirumba.

“Tulianza wao wamefuata tusubiri dakika 90 zitaamua ubora wetu na wao wanaoamini ndio wamestahili na sisi hatukupaswa kucheza hiyo hatua tumefurahia ratiba kwasababu kila timu kwetu tunaipa ubora bila kujali wamepataje nafasi ya kutinga hatua hiyo,” alisema na kuongeza:

“Tumecheza mechi tatu msimu huu na Simba tumeshinda mechi moja ya ngao ya jamii mbili zote tumeambulia suluhu hivyo kuelekea mchezo ujao makocha wote watakuwa na mbinu mbadala ili kuhakikisha matokeo yanapatikana na atakayeibuka mshindi ndiye atacheza fainali.”

Wakati huohuo, winga, Farid Mussa alisema maneno na mpira ni vitu viwili tofauti wamekisikia kilichozungumzwa hawakipi kipaumbele zaidi wanajipanga kuhakikisha wanakuwa bora ili kumkata kilimi kocha huyo ambaye anaamini hawastahili.

“Mpira ni mchezo wa wazi kila mmoja aliona kilichotokea dhidi yetu na Geita Gold hivyo hadi kutinga hatua hiyo ni wazi kuwa tulistahili kazungumza sisi tutatenda kwa vitendo nusu fainali kwani tunahitaji kucheza fainali ili kutimiza malengo ya kutwaa mataji yote msimu huu.”

Naye Dickson Job alisema mti wenye matunda ndio unapigwa mawe hivyo kauli zinazozungumzwa dhidi yao ni kutokana na ubora walionao hawatishi wataendelea kuwa bora ili waendelee kusikia kauli kama hizo.

“Tunawaheshimu tunaichukulia kauli yao kama changamoto kwa kujifua zaidi ili baada ya dakika 90 tumpe maswali ya kujiuliza na sio maneno kama aliyoyazungumza sasa.” alisema.

Wakati wachezaji wakizungumza hayo Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Klabu ya Yanga, Hersi Said alisema malengo hayo hayajabadilika ni kutwaa mataji yote wanayoyashiriki Tanzania bila kujali nini kinazungumzwa huku akisisitiza ushindi dhidi ya Dodoma ni mwendelezo kwenye mechi zote zilizo mbele yao.

“Hatutetereki ndio kwanza tunaongezwa nguvu kama wanatamka hivyo wakiamini tutarudi nyuma watafute mbinu nyingine ndio kwanza wametuongeza nguvu za kuendelea kujiimarisha msimu huu tunataka mataji na tunatimu iliyo imara,” alisema.

“Tumekutana nao mara tatu hadi sasa sisi tumechukua pointi tano sitaki kuzungumzia kwa upande wao wamepata ngapi ila awamu hii aliye bora ndiye atakayecheza fainali tukutane CCM Kirumba,” alisema kiongozi huyo aliyehusika na asilimia kubwa ya usajili wa mastaa wa Yanga.


SIMBA, YANGA WA MBEYA

Shabiki na mwenezi wa Yanga Mbeya Mjini, Said Walilo alisema msimu huu hawataki kuacha kitu, akisema kuwa wanataka kulipa kisasi kama walivyofanya watani zao msimu uliopita kwa kubeba makombe yote.

“Si wamejileta wao, acha waje na tusilaumiane, msimu huu riziki ipo kwetu tutabeba kila kitu, naamini kazi watakayokutana nayo Mwanza hawatasahau, sisi mashabiki tutaendelea kuiombea na kuisapoti Yanga yetu,” alisema Walilo.

Naye Ramadhan Mwaisango shabiki wa kufa wa Simba Jijini hapa, alisema bado nafasi ya Wekundu kutetea mataji yao yako wazi, huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo.

“Iwe Ligi Kuu, kombe la Shirikisho sisi ndio tutaamua, tunawasubiri Mwanza ili waje ila tunawatahadharisha tusije kulaumiana kwa sababu hii ni mechi ya wakubwa,” alitamba Mwaisango.