Yanga walijiamini balaa

Muktasari:

YANGA jana walionekana kujiamini zaidi kuliko Simba katika mpambano wao wa mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambao ulipaswa kuchezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, kabla ya kuahirishwa baada ya Yanga kuondoka uwanjani wakidai kupindishwa kwa taratibu za muda wa kuanza.

YANGA jana walionekana kujiamini zaidi kuliko Simba katika mpambano wao wa mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambao ulipaswa kuchezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, kabla ya kuahirishwa baada ya Yanga kuondoka uwanjani wakidai kupindishwa kwa taratibu za muda wa kuanza.

Kujiamini kwa mashabiki wa Yanga kulitokana na kikosi chao kilivyokuwa wakiamini kingewapa matokeo mazuri.

Mashabiki wa Yanga wakilalamika baada ya muda wa mechi yao dhidi ya Simba kusogezwa mbele. Picha na Michael Matemanga

Wanachama na mashabiki wa Yanga kutoka tawi la Mtogole walikuwa na uhakika wa matokeo mazuri ya mchezo huo, licha ya kukiri kwamba Simba ni bora kuliko wao, ila ubora huo hauwatishi kuchukua pointi tatu.

Shecky Ambrose alisema hawana wasiwasi na mchezo kwa kuwa uwezo wa wachezaji wao uko juu na hawawezi kuwahofia watani zao.

“Yanga hatuna shida kabisa na wala hakuna mwenye wasiwasi wa namna yoyote ile na tunashinda mchezo, “ alisema shabiki Abeid Khamis huku akisisitiza walichokuwa wanakihofia ni wakali wa Simba, Clatous Chama na Luis Miquissone peke yao.

“Luis na Chama ndio wanatakiwa kuchungwa, hawa hawastahili kucheza Simba kabisa, wanatakiwa kuwa Yanga hawa.

“ Tuna uhakika uwezo tunao, hata kama (Simba) wanatamba wana uwezo mbona tumewasumbua michezo ya nyuma, tumedroo na tumewafunga wakaona wamchukue Bernard Morrison.”

Fatma Shaban alisema kikosi chao pia kina nyota wakali huku akimtaja Tuisila Kisinda ndiye angewalaza na viatu Simba. “Yanga hii daima mbele nyuma mwiko, hakuna wa kututisha, ndio maana unaona tuko vizuri tunatamba sana,” amesema.