Yanga wahamishiwa uwanja wa kitajiri, Nabi arudisha dozi

TIMU nzima ya Yanga kuanzia juzi mchana walikuwa katika mapumziko mafupi wakiwasubiri wenzao waliokuwa katika majukumu ya kimataifa na jana walirudi, lakini watakutana na ratiba ngumu ya dozi mara mbili kwa siku.

Kocha Nesreddine Nabi amesisitiza kwamba hataki kumuona mchezaji yeyote anakosekana katika ratiba ya leo akitaka dozi ambayo wanakwenda kuitoa sasa imuingie kila nyota wa kikosi chake.

Habari za ndani zinasema kwamba hata viongozi walikuwa wakiwasisitiza wachezaji kila mmoja kuwahi kwa wakati kambini na kufuata maelekezo kama programu ilivyopangwa na watapashia kwenye gym ya viwanja ghali vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema alilazimika kuwapa mapumziko wachezaji wake ambao walisalia katika timu baada ya kuona walifanya mazoezi makali takribani wiki moja akishtukia wanaweza kukumbana na ‘fatiki’ kama wangeendelea na mazoezi.

Nabi alisema anaamini mapumziko ya siku moja na nusu yatawarejeshea utulivu wachezaji wake na kwamba leo watarudi tena kwa nguvu wakianzia gym kisha baadaye jioni kazi itarejea uwanjani kwenye dozi ya kucheka na nyavu.

“Tulikuwa na kundi ambalo halikuwa katika majukumu ya timu za taifa tulifanya kazi nzito sana ndani ya wiki na baada ya mchezo wa kirafiki tuliendelea nao,tumeona tuwape mapumziko ya kama siku moja,” alisema Nabi.

“Tutarudi mazoezini lakini hapa sasa nimewaambia sihitaji dharura nataka kila mchezaji awepo tumetoa mapumziko haya ili hata wale waliokuwa wanarejea wawe wamefika tuendelee na ratiba hii tukiwa pamoja,”alisema

Nabi alisema ameonyeshwa aina ya uwanja ambao wanakwenda kuutumia lakini pia anajua aina ya timu ambayo wanakwenda kukutana nayo ambapo lazima wawe na maandalizi ya nguvu ambayo yatakwenda kuwapa matokeo wanayoyataka.

“Tunatakiwa kusafiri kuwafuata KMC nimeonyeshwa aina ya uwanja ambao tutakwenda kuutumia nafikiri malengo yako kuupeleka mchezo huu huko lakini pia aina ya timu ambayo tunakwenda kukutana nayo ni muhimu tukawa na maandalizi ya aina hii ambayo tunayafanya sasa.

“Tunahitaji kushinda hiyo mechi hatuwezi kushinda kwa ukubwa wa jina la klabu tunatakiwa kuwa bora uwanjani na ndio maana nataka ratiba ya kila mchezaji aihudhurie tuwe na ubora unaolingana.”

Yanga katika mechi zake mbili zilizopita za ligi haijapoteza wakiwa na pointi sita lakini pia ikifunga kila mechi bao moja na sasa wanakwenda kukutana na KMC ya kipa mzoefu na mwenye jina kubwa nchini, Juma Kaseja.

Aliyekuwa Kocha msaidizi wa Gwambina FC, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema aina hiyo ya mazoezi inawasaidia wachezaji kuongeza nguvu mwilini wakati wanapopambana na timu zenye matumizi makubwa ya nguvu.

“Inategemea kocha anahitaji nini kutoka kwa wachezaji wake lakini ukiangalia hali kama hiyo mwalimu anahitaji kuwapatia stamina ili baadae kuwarahisishia wakati wa kufanya mazoezi mepesi, lengo ni kuwajengea utimamu wa kimwili,” alisema.

Yanga wamepania kushinda mechi hiyo ya KMC ili kupata kasi ya kuwakabili Azam kwenye mechi itakayofuata Jijini Arusha ambayo inatazamiwa na yenyewe kuwa na ushindani mkubwa kutokana na usajili na ushindani wa timu hizo.

Azam inanolewa na George Lwandamina ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga.