Yanga Princess yataka 3 bora

KOCHA wa Yanga Princess, Sebastian Nkoma amesema wamejipanga kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) katika nafasi tatu za juu.

Timu hiyo hadi sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13, imeshinda michezo minne, imefungwa mmoja na kutoka sare mmoja, imefunga mabao 13 na kufungwa mabao matano.

Hadi sasa JKT Queens inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 16 ikifuatiwa na Fountain Gate Princess yenye pointi 15 na Simba Queens inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 13 huku Mkwawa Queens ikiburuza mkia ikiwa na pointi moja.

Timu hiyo imeshinda dhidi ya Baobab Queens 2-1 (Jamhuri Dodoma), Ceasiaa Queens 1-0 (Chuo cha Mkwawa Iringa) Mkwawa Queens 4-0 (Uhuru) imefungwa na Fountain Gate Princess 1-0 (Uhuru) na imetoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Simba Princess (Mkapa).

Timu hiyo imebakisha michezo mitatu kumaliza mzunguko wa kwanza na Februari Mosi mwaka huu itacheza dhidi ya JKT Queens katika Uwanja wa Meja General Isamuhyo kisha itacheza na The Tiger Februari 7 mwaka huu na itamaliza michezo yake ya mzunguko wa kwanza Februari 15 mwaka huu dhidi ya Amani Queens kwenye Uwanja wa Uhuru.

Nkoma alisema anashukuru timu yake kupata matokeo katika michezo miwili ya ugenini dhidi ya Baobab Queens na Ceasiaa Queens.

“Baada ya hapo tutajipanga sasa kwa mzunguko wa pili na tutajua tupo kwenye mbio za ubingwa ama hapana,” alisema kocha huyo ambaye msimu uliopita aliipa ubingwa Simba Queens.