Yanga Princess yajituliza nafasi ya tatu WPL, mbili zashuka daraja

Mwanza. Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) msimu wa 2021/2022 imehitimishwa rasmi leo Mei 20 kwa michezo yote sita ya raundi ya mwisho kupigwa huku Yanga Princess ikikwaa kisiki jijini Mwanza.

Yanga Princess ambayo msimu uliopita ilimaliza kwenye nafasi ya pili nyuma ya bingwa  Simba, msimu huu imejikuta ikishuka kwa nafasi moja na kumaliza ya tatu huku Simba Queens ikiwa mabingwa na Fountain Gate Princess ikishika nafasi ya pili.

Yanga imekwama leo katika uwanja wa Nyamagana jijini hapa baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Alliance Girls hivyo kufikisha pointi 54 sawa na Fountain Gate huku matajiri hao wa Dodoma wakiwa na faida ya mabao ya kufungwa na kufunga.

Yanga Princess yajituliza nafasi ya tatu WPL, mbili zashuka daraja

Yanga Princess ilikuwa ya kwanza kupata bao mnamo dakika ya 60 likifungwa na Amina Ally na kuwafanya wajiamini kwani ushindi ungewahakikishia nafasi ya pili lakini bao la dakika ya 90 lililofungwa na Winfrida Charles likazima ndoto hizo.

Katika michezo mingine Simba Queens imenogesha sherehe zao za ubingwa kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Baobab Queens katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mabao yakifungwa na Asha Djafari, Joelle Bukuru na Pambani Kuzoya.

Fountain Gate Princess imejihakikishia nafasi ya pili baada ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya maafande wa JKT Queens bao pekee likifungwa na mkongo S'arrive Bandiambila huku TSC Queens wakipigwa 3-2 na Ilala Queens.

Timu mbili za TSC Queens ya Mwanza ambayo imemaliza na alama saba na Oysterbay Girls ya jijini Dar es Salaam yenye pointi 15 zimeshuka daraja huku Ilala Queens (15) na Mlandizi Queens ya Pwani yenye pointi 19 zikisubiria hatma yao kama nazo zitashuka moja kwa moja ama zitalazimika kucheza mtoano (playoff).