Yanga: Njooni mhesabu pasi

MASHABIKI wa Yanga wameitwa Kwa Mkapa, ili kuhesabu pasi na mabao wakati kikiosi chao kitakapocheza mechi yao ya kwanza wa Ligi Kuu Bara kwenye uwanja wa nyumbani ikiikaribisha Geita Gold ya Geita mchezo utakaopigwa kuanza saa 1:00 usiku.

Vichwani mwa mashabiki wa Yanga, neno ushindi tu ndilo linalotawala wakijianda kuishuhudia chama lao likivaana na wageni hao wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, hii ikiwa ni baada ya kunogewa na ushindi mfululizo iliyopata timu yao katika mechi mbili zilizopita ukiwamo wa Ngao ya Jamii.

Mchezo huo wa Dar ni kati ya mechi tatu za ligi zinazopigwa leo ukiwamo ule wa mjini Moshi wakati Polisi Tanzania itakayovaana na Azam na mapema mchana Wagosi wa Kaya, Coastal Union itaumana na KMC kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Licha ya kuwepo kwa mechi hizo, lakini akili za mashabiki wengi wa soka wataifuatilia zaidi Yanga kutaka kuona kama itaendeleza moto iliyoanza nayo katika Ligi kwa kuifunga Kagera Sugar siku chache tangu ilipoifunga Simba katika Ngao ya Jamii, iliyozindua msimu mpya.

Mashabiki wa Yanga wana kiu ya kutaka kuona timu yao inazoa alama nyingine tatu ili kutengeneza pengo baina yao na wapinzani wakuu kwenye ubingwa, Simba na Azam zilizoanza na sare mechi zao za awali.

Na hilo linachagizwa zaidi na kuimarika kwa timu yao hasa katika utengenezaji wa nafasi za mabao msimu huu kulinganisha na ule uliopita ambapo ilikuwa ikihaha katika eneo hilo.

Lakini kiwango kizuri na ufanisi wa mchezaji mmojammoja ambao umeonyeshwa katika mechi walizocheza hivi karibuni ni jambo lingine ambalo bila shaka linawafanya Wanayanga wahitaji matokeo mazuri mbele ya Geita Gold leo na sio vinginevyo, na ndio maana Wasemaji wa timu hiyo, Hassan Bumbuli na Haji Manara wamewaita waenda Kwa Mkapa.

Manara na Bumbuli walisema kwa muda tofauti katika mkutano wao wa jana kuwa, kwa namna Yanga yao ilivyo kwa sasa kwa kupiga pasi nyingi na kufunga, wanawataka mashabiki wao wajitokeze kwa wingi ili wazihesabu pamoja pasi hizo zitakazoenda sambamba na mabao ya kuwapa ushindi kwa vile msimu wanataka kurudisha heshima yao waliyoipoteza kwa misimu minne mfululizo mbele ya watani wao Simba.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wenyeji, Geita inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, ikihitaji ushindi ili kujiondoa katika uwezekano wa kuwa na mwanzo mbaya katika msimu huu hasa baada ya kuanza kwa kupoteza mechi ya Namungo FC, Jumatatu iliyopita kwa mabao 2-0.

Uwepo wa wachezaji na makocha wazoefu wa Ligi Kuu katika kikosi chao ni jambo ambalo bila shaka linaweza kuwasaidia Geita Gold kupambana na Yanga ambayo inaonekana kuimarika vilivyo.

Kocha Etienne Ndayiragije aliwahi kuzinoa Mbao FC, KMC na Azam FC na msaidizi wake Felix Minziro amewahi kucheza na kuinoa Yanga, ingawa ameshawahi kuzifundisha pia Prisons, JKT Ruvu na Moro United na mfano wa wachezaji wazoefu waliopo kikosini ni pamoja na Danny Lyanga, Maka Edward, Idd Mobby na Benedictor Tinoco.

Yanga inaingia katika mechi ya leo ikiwa inajivunia rekodi ya kufanya vizuri katika mechi za nyumbani za Ligi Kuu ambapo mara kwa mara imekuwa ikipata ushindi huku ikiwa ni nadra kupoteza.

Katika mechi 30 zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo Yanga ilikuwa nyumbani, imeibuka na ushindi mara 18, kutoka sare michezo 10 na kupoteza mechi tatu tu.

Yanga katima mchezo wa leo itaendelea kuwakosa Mapinduzi Balama na Yassin Mustafa ambao bado hawako fiti baada ya kupona majeraha yao ya muda mrefu, Bakari Mwamnyeto ambaye ni majeruhi pamoja na Tonombe Mukoko anayemalizia adhabu ya kukosa mechi tatu huku nyota wengine wa kikosi hicho wakiwa fiti.

Kocha msaidizi wa Geita Gold, Felix Minziro alisema wamejiandaa vyema kwa ajili ya mechi hiyo ambayo wanaamini itakuwa ya aina yake.

“Vijana wangu naamini watasahau matokeo ya mchezo uliopita baada ya kupoteza na Namungo na tutakwenda kupambana ili kupata matokeo mazuri katika mchezo huo,” alisema Minziro.

Kwa upande wa Yanga, Mkuu wa Idara ya Habari wake, Hassan Bumbuli alisema kuwa wako tayari kwa mchezo huo na wamejipanga kuhakikisha wanashinda.

“Kocha amesema niwaambie kuwa timu iko vizuri na imejipanga kushinda licha ya kwamba mchezo utakuwa mgumu,” alisema Bumbuli, huku Manara aksisitiza ufalme wa Yanga unarejeshwa msimu huu na dalili zimeonekana kwa kuanza na Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba, aliodai ndio timu waliyoifunga zaidi.

Ukiachana na rekodi za mechi za michuano mingine ikiwamo ya Ngao ya Jamii, Kombe la ASFC, Yanga na Simba zimekutana katika Ligi ya Bara mara 106 tangu ligi ilipoasisiwa mwaka 1965 na Yanga kushinda 38, huku Simba ikishinda 31 na mechi zao 37zikiisha kwa sare mbalimbali kuthibitisha tambo za Manara kwamba Yanga ndio klabu pekee duniani iliyoifunga mara nyingi Simba kuliko yoyote.


Mechi nyingine

Kabla ya patashika hiyo ya Dar, Coastal itaialika KMC, huku wageni wao kupitia Ofisa Habari wao, Christina Mwagala alisema benchi lao la ufundi limewahakikisha leo Mkwakwani wanasahihisha makosa.

Nako kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi Azam itakuwa ikijiuliza mbele ya wenyeji Polisi Tanzania.