Yanga ni Job, halafu wengine

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amefichua kukipangua kikosi chake wakati akiikabili Geita Gold leo katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku akihakikishia nafasi beki wake wa kati Dickson Job, aliyedai kiwango bora kimempa nafasi kubwa ndani ya kikosi chake licha ya kuwepo kwa maingizo mapya kwa sasa.

Job aliyesajiliwa dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar, amekuwa mmoja wa mihimili ya ukuta wa Yanga unaoundwa pia na nahodha Bakar Mwamnyeto, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Yannick Bangala. Wakati akiingia kikosini, Job alicheza na Lamine Moro kisha akapewa Mwamnyeto na Ninja na kuna wakati akicheza na Said Juma ‘Makapu’ aliyepo Polisi Tanzania kwa sasa na juzi dhidi ya Kagera alianza na Bangala na kutengeneza ukuta mgumu uliolindwa vyema na kiungo Khalid Aucho.

Tuanze na ishu ya kikosi. Nabi alisema mchezo wa leo, atafanya mabadiliko ya baadhi ya nyota kutokana na kutumia nguvu nyingi katika michezo miwili iliyopita.

Alisema kutokana na mambo hayo, leo atakipangua kikosi, lakini akisema kwa mara ya kwanza alivutiwa na Job aliyeingia katika kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa kwa umakini mazoezini na hata uwanjani.

“Kwanza ukimuangalia kimo chake na kazi ambayo anafanya uwanjani ni vitu viwili tofauti anapenda kujituma na kufuata maelekezo ambayo kila siku huwa nampatia katika mazoezi na mechi,” alisema Nabi


MSIKIE JOB

Job alisema tangu amesajiliwa Yanga kuna mabadiliko ya makocha yamefanyika, lakini kutokana na kujituma, kufanya mazoezi na kuwasikiliza wanaendelea kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza. “Nimecheza na Bakari Mwamnyeto na Yannick Bangala kwa nyakati tofauti katika eneo la mabeki wa kati binafsi naona wote sawa.”