VIDEO: Yanga kujenga uwanja Jangwani

Yanga kujenga uwanja Jangwani

Muktasari:

  • Hersi amefungua kampeni zake kwenye ukumbi wa hoteli ya Serena Dar es Salaam akiwa ameambatana na mgombea wa umakamu wa rais, Arafat Haji.

Mgombea urais wa klabu ya Yanga, injinia Hersi Said ametaja vipaumbele sita endapo atapewa ridhaa ya kuwa rais wa klabu hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa Julai 9.

Amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kuboresha miundo mbinu.

Katika ufunguzi wa kampeni zake, Hersi ameadhidi kuanzisha mchakato wa kuijengea uwanja timu hiyo utakaobeba watu elfu ishirini katika eneo la Kaunda lililopo Jangwani.

"Eneo la pili kwenye miundo mbinu ni ardhi ya klabu iliyopo Kigamboni, ambako nina plani ya kutengeneza training center, lakini pia kuboresha jengo letu la Jangwani.

"Kipaumbele cha pili ni mabadiliko ya uendeshaji wa klabu, mimi ni muumini wa mabadiliko na nikipewa nafasi nitayasimamia kivitendo," amesema Hersi

Amesema katika eneo hilo umiliki wa klabu ni asilimia 51 na wawekezaji asilimia 49.

"Katika kipaumbele hicho nitasimamia muundo wa klabu ambayo inafungua nguzo tatu, kuwa na bodi, kulinda maslahi ya klabu na kuwa na excom.

"Pia kuwaalika wawekezaji kuwa kwenye klabu, kuithaminisha klabu na kupata thamani yake na kufungua kampuni.

VIDEO: Yanga kujenga uwanja Jangwani

"Bodi itakuwa na watu tisa, watano kutoka kwenye klabu," amesema.

Amesema kipaumbele cha tatu ni kuimarisha uchumi wa klabu akifafanua kwamba miaka kadhaa nyuma klabu iliyumba kwa kuwa haikuwa na uchumi imara.

"Tutaimarisha miradi kupitia usajili wa wanachama na mashabiki, wadhamini, na kuwa na mazingira yakuwavutia wawekezaji". amesema Hersi

Kipaumbele cha nne ni ubingwa ambao amesema kama akipewa ridhaa, atahakikisha klabu inapata mafanikio kwa kushinda Mapinduzi, FA, Ligi Kuu, Ngao ya hisani na kufika mbali kimataifa.

"Msimu huu Yanga tumeshinda Ngao ya Hisani, FA na Ligi Kuu nikiwa sehemu ya mafanikio hayo," amesema.

Ametaja kipaumbele cha tano kuwa ni kujenga timu zote ndogo za klabu ili kuleta mchango kwenye timu ya wakubwa.

"Yanga princes haijawahi chukua ubingwa kwenye Ligi kuu ya wanawake, hivyo nikipewa ridhaa nitahakikisha pia inapata mafanikio.

"Kipaumbele changi cha sita ni kujenga ushirikiano wa klabu, wanachama, mashabiki na washika dau," amesema Hersi.