Wydad yachezea kipigo nyumbani

Muktasari:

MIAMBA ya soka ya Morocco, Wydad Casablanca anayoichezea Mtanzania, Simon Msuva imeanza vibaya mchezo wa kwanza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs.

MIAMBA ya soka ya Morocco, Wydad Casablanca anayoichezea Mtanzania, Simon Msuva imeanza vibaya mchezo wa kwanza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs.

Katika mchezo huo, kocha wa Wydad Casablanca, Faouzi Benzarti aliamua kuingia na mfumo wa 4-2-3-1 huku akiamua kuanza na Ounajem, El Karti na Ellafi kama viungo washambuliaji huku mmoja kati yao akiwa na jukumu la kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho, El Kaabi.

Kitendo cha kuanza na viungo hao washambuliaji hasa waliokuwa wakitokea pembeni maarufu kama mawinga, Ounajem na Ellafi, kilibeba tafsiri kuwa Benzarti aliona kama Msuva akitokea benchi kwenye mchezo huo anaweza kuongeza nguvu ya mashambulizi.

Kwa upande wa Kaizer Chiefs wakiwa na kocha wao mpya, Arthur Zwane ikiwa ni wiki chache tu tangu kutimuliwa kwa Gavin Hunt, waliingia na mfumo wa 3-4-1-2 ambao uliwanyima uhuru Wydad wa kufika zaidi kwenye eneo lao kutokana na idadi na mabeki ambao walikuwa wakicheza nyuma, walionekana watatu wa kati lakini walikuwepo wengine pembeni.

Wydad Casablanca walijitahidi kuwa na umiliki mkubwa wa mpira lakini Kiazer Cheifs walifunga njia zote za wao kupenya, vijana wa Zwane walikuwa na hesabu kuwashambulia kwa kustukiza na mbinu hizo zilikuwafanya kuwa hatari.

Dakika ya 35, mbaya wa Simba SC kwenye mchezo wa robo fainali ya kwanza iliyochezwa Afrika Kusini, Samir Nurkovic aliwafanya kitu mbaya Wydad Casablanca, bao hilo liliamuliwa baada ya kutazamwa vizuri na VAR maana ilionekana ni kama mfungaji aliotea kabla ya kufunga.

Baada ya sekunde chache mwamuzi, Maguette N’Diaye alisema lilikuwa bao halali na mfungaji hakuwa amejenga kibanda, aliutegua vizuri mtego wa kuotea na kuitanguliza Kaizer Chiefs.

Kocha wa Wydad aliamua kufanya mabadiliko kadhaa kipindi cha pili ili kuona kama wanaweza kukomboa bao ambalo walikuwa wametanguliwa, ikiwemo kuingia kwa Msuva lakini mabadiliko hayo hayakubadili chochote kwani Kaizer walitengeneza ukuta wa chuma na mchezo huo umalizika kwa wenyeji kupoteza kwa bao la Nurkovic lililofungwa kipindi cha kwanza.

Kwa maana hiyo kina Msuva wana kibarua kizito cha kwenda kupindua meza Afrika Kusini ili kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika ngazi ya klabu.

Mchezo wa nusu fainali ya pili ilishuhudiwa mabingwa watetezi Al Ahly wakiichapa Esperance ya Tunisia wakiwa ugenini.

Michezo ya marudiano inatarajiwa kuchezwa Juni 26 huku fainali ambayo itahusisha washindi wa jumla ikitarajiwa kuchezwa Julai 17 kwenye Uwanja wa Stade Mohammed V ambao umekuwa ukitumiwa na Wydad Casablanca na Raja Casablanca za Morocco.