Winga wa Simba kama Clatous Chama

Monday October 05 2020
juma chama pic

WINGA wa Simba anayekipiga kwa mkopo Polisi Tanzania, Rashid Juma amesema amepewa jukumu maalum la kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri, huku akidai anapita mulemule anapopita Clatous Chama ndani ya Msimbazi.

Juma alisema akiwa Simba alikuwa anamuiga Chama, anayepewa majukumu ya kuwa mchezaji anayehusika kwa kiasi kikubwa kutengeneza mashambulizi na nafasi za kufunga, kitu ambacho anafanya sasa.

“Ukiangalia kwa makini tunavyocheza wakati huu Polisi Tanzania utaona nahusika katika mashambulizi mengi yawe yamezaa bao au tumeshindwa kufunga, hii kazi niliyopewa na Kocha Malale Hamsini,” alisema Rashid na kuongeza;

“Kama timu ikiweza kufanya vizuri kutokana na kutimiza majukumu yangu basi hata mwenyewe nitakuwa nimejitangaza na naweza kuwa na biashara nzuri mwisho wa msimu kwani nitakuwa mchezaji huru.”

Rashid anatarajiwa kuwepo kwenye kikosi cha timu yake ambayo leo kitakuwa kikivaana na wenyeji wao KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, huku wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zote mbili za msimu uliopita.

Advertisement