Watatu Dodoma Jiji kuikosa Yanga

JOTO la mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Dodoma Jiji na Yanga Sc linazidi kupanda huku wenyeji wakitarajiwa kuwakosa nyota wake watatu katika mtanange huo.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa leo Jumanne kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida ambapo Chama cha Soka mkoani wa Singida (Sirefa) kupitia Katibu Mkuu, Juma Mwendwa kimesema maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika.

Dodoma Jiji  inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 9 ikishuka dimbani mara 11 huku Yanga ikishika nafasi ya pili na zake pointi 26 ikiwa imecheza michezo 10.

Mchezo wa mwisho Dodoma Jiji iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Uhuru Jiji Dar es salaam huku Yanga ikiibutua Singida Big Stars mabao 4-1 kipute kilichofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Klabu hizo ziko katika ushindani mkali katika nafasi zao wakati Yanga ikiwa inataka kutetea ubingwa wake, Dodoma Jiji inapambana kujinasua kutoka chini ya msimamo ili isiweze kucheza play off au kushuka daraja.

Daktari wa Dodoma Jiji, Baraka Edwin alisema wachezaji Jimmy Shoji, Abubakari Ngalema na Joram Mgeveke wanatarajia kuukosa mchezo huo kutokana na kuumia.

Alisema Shoji aliumia katika mchezo dhidi ya KMC pamoja na Mgeveke huku Ngalema akiwa na majeraha ya muda mrefu.

Katika hatua nyingine daktari huyo alisema mshambuliaji wa klabu hiyo, Salim Kihimbwa ameanza mazoezi na wenzake na Kocha Melis Medo ana uwezo wa kumtumia katika mchezo huo.

Kocha Medo alisema mchezo huo utakuwa mgumu lakini mategemeo yake ni kupata pointi tatu.


ISHU YA SHOJI

Kiungo Shoji atakuwa nje kwa takribani miezi mitatu baada ya kufanyiwa operesheni ya goti aliloumia katika mchezo wa KMC.

Shoji aliumia katika dakika ya 40 ya mchezo huo na kutolewa kwa machela baada ya kugongana na George Makang’a wa KMC kisha alipakizwa kwenye gari la wagonjwa na kuwahishwa hospitalini.

Edwin alisema Shoji baada ya kuumia alifanyiwa uchunguzi wa haraka na kugundulika kupata shida kwenye goti lake.

“Tulimuangalia kwa umakini na leo Jumamosi (juzi) ndio ameruhusiwa kutoka baada ya kufanyiwa upasuaji, atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu hadi minne,” alisema Edwin.

Kukosekana kwa Shoji ambaye alikuwa anaanza kwenye kikosi cha kwanza ha Kocha Medo kunatoa fursa kwa Rajab Mgalula ambaye huwa anakaa benchi na aliingia kwenye mechi ambayo Shoji aliumia.

Shoji akiwa uwanjani akiitumikia Dodoma Jiji amekuwa kiongozi kutokana na uzoefu wake alionao wa kucheza Ligi Kuu huku akisifika kwa uwezo wa kupiga pasi ndefu ambazo zinafika kwa wahusika.

Shoji alijiunga na Dodoma Jiji msimu huu akiwa mchezaji huru baada ya klabu yake ya Mbeya Kwanza kushuka daraja.