Wasikie mashabiki kijiweni kuhusu Kariakoo Dabi

Muktasari:

Mwanaspoti limetia timu katika kijiwe cha Tandale kwa Tumbo, Dar es Salaam na kukuta ubishi mkali wa mashabiki wa Simba na Yanga, kutokana na kuahirishwa mechi ya Dabi ya Simba na Yanga.

Mwanaspoti limetia timu katika kijiwe cha Tandale kwa Tumbo, Dar es Salaam na kukuta ubishi mkali wa mashabiki wa Simba na Yanga, kutokana na kuahirishwa mechi ya Dabi ya Simba na Yanga.

Simba na Yanga zilikuwa zicheze jana Jumamosi Mei 08, 2021 saa 11:00 jioni lakini badae ukasogezwa muda hadi 1:00 usiku kabla ya mchezo huo kuahirishwa.

Leo Jumapili Mwanaspoti limepata fursa ya kuzungumza nao mawili,matatu,huku kila shabiki akivutia kwamba kwa upande wake kuona yupo sahihi.

Miraji Mtibwiriko ni shabiki wa Simba lialia kwa upande wake ameona Yanga imekimbia mchezo, walijua watapigwa ndio maana hawakuta kujipa subra.

"Japokuwa siungi mkono walichokifanya TFF na Wizara ya Michezo, lakini Yanga wasingekubali kuondoka wakati maandalizi yamefanyika wiki nzima, mpira unachezwa eneo la wazi, angejulikana nani kajiandaa zaidi,"amesema na kuongeza kuwa;

"Simba mechi ya Dabi ilikuwa ya kujiandaa na Kaizer Chiefs, kitendo cha wao kutukimbia wametuzingua sisi na Watanzania ambao walitamani kuona ushindani huo,ina maana wangechezana Ihefu ama Gwambina wangekimbia,"amesema.

Kwa upande wa shabiki wa Yanga, Sadaty Kulachi amesema lawama anazielekeza kwa vyombo vinavyosimamia soka kushindwa kuheshimu kanuni za soka.

"Mabadiliko ya muda yanatakiwa yafanyike angalau massa 24 kabla ya mechi,sasa wanakuja kusema ndani ya masaa mawili huko nikutukosea, hili liwe mwanzo na mwisho na turudishiwe gharama zetu,"amesema.

Shabiki mwingine wa Simba, Said Omary ambaye amesema ametoka Afrika Kusini mji wa Dabani, kuangalia mchezo huo,ameudhika namna alivyopotezewa muda.

"Mimi ni Mtanzania naishi Afrika Kusini katika mji wa Dabani huko nimeenda kutafuta maisha, imenikosti gharama,muda yaani inakela sana na hao waliotoka mikoani je,TFF waliangalie hilo lisijirudie,"amesema.