Wana jambo lao VPL

Muktasari:

UKIACHANA na kitendawili cha timu gani itachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, upande mwingine mgumu wa ushindani wa straika nani ataibuka kinara wa mabao mengi ya kumpa kiatu cha dhahabu.

UKIACHANA na kitendawili cha timu gani itachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, upande mwingine mgumu wa ushindani wa straika nani ataibuka kinara wa mabao mengi ya kumpa kiatu cha dhahabu.

Ndani ya misimu miwili mfululizo, straika wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere aliweka utawala wake, alimaliza na mabao 23 (2018/19) na mabao 22 (2019/20) ligi inayoendelea kwasasa ana mabao tisa.

Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya washambuliaji ambao msimu ulioisha walifunga mabao mengi na kujua endapo msimu huu wanaweza wakavunja rekodi zao ama kufanya maajabu mengine zaidi.

Kagere alisema malengo yake makuu ni kufikia idadi ya mabao 22 ya msimu ulioisha, akikamilisha hilo ataanza kupambania kuweka rekodi nyingine kwa msimu huu, akiwa chini ya kocha Didier Gomes ambaye hampi sana nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

“Ninaanza na kuifikia idadi ya mabao niliyomaliza nayo msimu ulioisha, sio kazi ndogo ila naamini katika kupambana kwamba hakuna linaloweza kushindikana,” alisema.

Peter Mapunda wakati yupo Mbeya City, alimaliza na mabao 13, lakini hadi sasa huko Dodoma Jiji ameifungia bao moja dhidi ya Ruvu Shooting, aliweka wazi kwamba hataweza kuwa kwenye nafasi ya kuvunja rekodi yake, kutokana na mazingira mapya ya kazi, pia hapati namba kikosi cha kwanza.

Licha ya kukiri hataweza kuvunja rekodi yake na kuwa miongoni mwa washambuliaji watakaofunga mabao mengi msimu huu, alimpa nafasi nahodha wa Simba, John Bocco kwamba anaweza akachukua kiatu cha ufungaji bora kama atakaza.

“Kilichonifanya niondoke kwenye mstari wa ushindani wa mabao ni mazingira mapya ya kazi, sipati nafasi mara kwa mara na mechi zimesalia chache, lakini mchezaji ninayemuona yupo vizuri zaidi ni Bocco atafanya makubwa zaidi,” alisema.

Straika wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu msimu ulioisha alimaliza na mabao 13 ambapo hadi sasa amefunga mabao sita, alizungumzia kuhusu kuvunja rekodi yake kwamba lolote linaweza kutokea.

“Sijakiri kushindwa kwasababu mechi bado zipo, napambana na ikiwezekana nifunge zaidi ya 13 ya msimu ulioisha kwani katika mpira lolote linawezekana,” alisema.

Mastaa wengine ambao walimaliza na mabao mengi ni Paul Nonga 11 akiwa Lipuli na sasa ana mabao (4 Gwambina), Daruweshi Saliboko, Lipuli alimaliza na mabao 11 (Polisi TZ mabao 4), Reliants Lusajo wa Namungo alimaliza na mabao 12 na sasa ana manne, Wazir Junior akiwa na Kagera Sugar alikuwa na mabao 13 (Yanga ana bao 1), Obrey Chirwa wa Azam alikuwa na mabao 12 na sasa na manne na Blaise Bigiramana wa Namungo alikuwa na mabao 10, sasa hajafunga.