Wadau wafunguka kuhusu uchaguzi TFF

WADAU wa soka kutoka maeneo ya Tabata, Relini jijini Dar wamesema hawaungi mkono suala la Rais wa shirikisho la soka Tanzania kuchaguliwa na wajumbe wachache na wamesisitiza kwamba suala hilo hufanya uchaguzi usiwe wa haki.
Akizungumza na Mwanaspoti mmoja ya wadau hao ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Pan Africa Allan Joseph alisema:"Wajumbe miaka yote ndio wale wale, mimi nashauri bora ziundwe kamati ambazo zitakuwa na watu wa mpira walau wa watano kwenye kila mkoa mbali ya wale wajumbe. Kwa sababu wanaomchagua rais ni watu wadogo ukilinganisha na wingi wa Watanzania ambao tupo zaidi ya milioni 50,
"Pia kwenye uchaguzi huu tunataka rais anayeujua vizuri mpira, hatutaki wajanja wajanja. Mtu awe na elimu ya mpira na ameucheza mpira, ukiangalia hata viongozi waliowahi kupita ambao walicheza mpira, waliongoza vizuri sana."
Mdau mwingine wa soka aitwaye Mohammed Nyama alifunguka kwa kusema:"Mimi naona uongozi ulio madarakani kwa sasa umeshindwa, ukianzia jinsi ligi ilivyoendeshwa. Suala lingine ni wajumbe, wajumbe ni wachache. Mimi nashauri walau wawachukue hata Makpteni wa timu mbali mbali ili waende kufanya uchaguzi. Kilio changu mimi ni wapiga kura waongezwe, wakiwa wachache inakuwa rahisi sana hata kununuliwa."
Vilevile Eliya Hamisi Michael alisema kilio chake kipo kwenye ratiba ya msimu huu, hivyo anaomba wale ambao watapata nafasi kuongoza shirikisho katika uchaguzi ujao waiondoe bodi ya ligi yote kwa sababu imeshindwa kusimamia soka, waondolewe tu na wachaguliwe wengine.
Uchaguzi huo wa Tff unatarajiwa kufanyika Agosti 7 mwaka huu na zoezi linaloendelea kwa sasa ni uchukuaji wa fomu.