Wachezaji Simba wajazwa manoti, mastaa wafunguka

Tuesday February 23 2021
manoti pic
By Clezencia Tryphone

BILIONEA wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ juzi alifanya kikao kizito na kuwawekea wachezaji Sh200 milioni mezani endapo watawapiga Al Ahly leo.

Taarifa ambazo Mwanaspoti lilizipata jana zinasema kuwa, Mo aliambatana na wajumbe wake wa bodi ya wakurugenzi pamoja na Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez.

Meddie Kagere alipoulizwa kuhusiana na uwepo wa zawadi hizo hakukiri, lakini alisema wao kama wachezaji licha ya bonasi wanazopewa na uongozi wao hatua waliyofikia hata wao wachezaji inawafanya kuzidi kujiuza na kujitangaza zaidi.

“Pesa tukishinda tunapata, lakini ushindi pia unatusaidia klabu yetu inazidi kujipatia wadhamini ambao wanaongeza mapato, mchezo huu tutahakikisha tunatimiza wajibu wetu,” alisema Kagere.

Larry Bwalya alisema wao kama wachezaji wanajua na kutambua majukumu yao ni yapi na watahakikisha wanapambana kupata matokeo ili mchezo wa marudiano wakapambane pia wakiwa na pointi tatu.

“Kama wachezaji tunayajua majukumu yetu, tunatamani sana kutwaa hili taji Afrika, nia na uwezo tunao tunamtanguliza Mungu tutafanya vizuri kesho,” alisema.

Advertisement

Lakini Thaddeo Lwanga alisema, “Al Ahly ni timu nzuri na kubwa lakini hata sisi Simba ni wazuri pia, tutahakikisha tunapambana kupata matokeo kesho.”

Beki kisiki, Erasto Nyoni aliwataka wachezaji wenzake kuwa na umoja na mshikamano ambao ndio suluhisho la kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Sisi kama wachezaji tunayajua majukumu yetu ni yapi na tutahakikisha tunayatimiza, kwa uwezo wa Mungu tutapata matokeo,” alisema.

Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema: “Tunatambua ubora wa Al Ahly ni timu ambayo inaongoza kwa ubora Afrika pia ni mabingwa watetezi wa michuano hii, tunawaheshimu lakini kutokana na mpira ni mchezo wa wazi tumejipanga kupambana nao ili tuweze kuibuka na ushidi muhimu kwenye uwanja wa nyumbani.”

Nahodha John bocco alisema: “Tumejiandaa kisaikolojia kuwakabili, pia tuna imani katika maandalizi tuliyofanya kuelekea mchezo huu, tunaenda kupambana nao huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atujalie tupate ushindi ambao ndio lengo letu sote.”

Mara ya mwisho timu hizi mbili kukutana ilikuwa Februari 12, 2019 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati huo ukiitwa Taifa na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, liliofungwa na mshambuliaji Meddie Kagere katika dakika ya 65.

Advertisement