Wababe wa Simba Queens kikaangoni Afrika

Muktasari:

  • Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake yanatarajiwa kufanyika huko Misri kuanzia Novemba hadi Disemba yakishirikisha jumla ya klabu nane kutoka Kanda tofauti za soka barani Afrika

Timu saba zitakazoungana na Vihiga Queens ambao ni wawakilishi wa Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya klabu bingwa Afrika kwa wanawake zitakazofantika mwezi Novemba hadi Desemba mwaka huu huko Misri zimejulikana baada ya kuibuka washindi katika kanda zao

Vihiga Queens ya Kenya ilitwaa ubingwa katika mashindano ya kuwania kufuzu mashindano hayo kwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika mwezi uliopita ambayo walikuwepo pia wawakilishi wa Tanzania, Simba Queens walioshika nafasi ya nne

Wawakilishi hao wa Afrika Mashariki wataenda kukutana na timu ambazo zinaonekana kuwa na uzoefu na mafanikio makubwa katika soka la wanawake kwenye nchi na kanda zao.

Mabingwa mara mbili wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Mali, AS Mande, washindi wa taji la Ligi Kuu ya Wanawake ya Nigeria mara saba, Rivers Angels na timu iliyotwaa taji la Ligi Kuu ya Wanawake ya Ghana, Hasaacas Ladies ni timu tatu ambazo zitaiwakilisha kanda ya Afrika Magharibi (WAFU)

Kanda ya Kusini itawakilishwa na washindi mara tatu wa taji la Ligi Kuu ya Wanawake ya Afrika Kusini, Manmelodi Sundowns na wataungana pia na timu ya AS Far ya Morocco ambayo ni bingwa wa mashindano ya kufuzu kwa kanda ya kaskazini

Kanda ya kati yenyewe itawakilishwa na timu ya Malabo King ya Guinea ya Ikweta wakati timu ya wanawake ya Wadi Degla yenyewe itashiriki mashindano hayo kutokana na nafasi ya uenyeji

Hii ni mara ya kwanza kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa na mashindano ya klabu bingwa ya wanawake