Wababe Simba wapewa mchongo kwa Kaizer Chiefs

VINARA wa Ligi Kuu Bara walio watetezi pia wa Kombe la Shirikisho (ASFC), Simba wamepewa mchongo wa kuwamaliza mapema wapinzani wao kwenye mechi za robo fainali, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini itakayopigwa kati ya Mei 14-22.

Simba itaanzia ugenini dhidi ya Mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Washindi wa Afrika 2001 katika mchezo wa kwanza utakaopigwa Mei 14 kabla ya kurudiana nao nyumbani wiki moja baadaye jijini Dar es Salaam kuamua hatma yao ya kutinga nussu finali.

Kuelekea mchezo huo, Wekundu hao wamepewa mchongo wa kujiandaa mapema dhidi ya Kaizer, ikiwamo kuweka kambi fupi ya kibabe nyumbani ili kwenda kumaliza mambo ugenini.

Kwa sasa Simba inajiandaa na mchezo wao dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, likiwa pambano lao la 106 katika Ligi Bara tangu 1965.

Mchongo huo wa kijanja, umetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Azam, Saad Kawemba aliyesema Simba haina sababu kubwa ya kuwahi kwenda Afrika Kusini ikiwa tu watajua wanacheza katika mji gani.

Kawemba alisema Kaizer wanaweza kuchagua kucheza Cape Town au Johanesburg, hivyo ni lazima wajiandae kwa mazingira yote mawili ili kupata matokeo mazuri ugenini kuwarahisishia kazi kabla ya kurudiana nao nyumbani baadaye.

“Katika miji yote hiyo miwili wanaweza kupata hali ya hewa inayofanana na miji hiyo hapa nyumbani, ipo mikoa inayolingana na hali ya hewa ya miji hiyo ya nyumbani ya Kaizer itakayowajenga kisaikolojia wachezaji wa Simba. Hawana haja ya kuwa na presha ya kukimbili kuwahi ugenini,” alisema Kawemba.

Kawemba alisema kitendo cha Simba kuanzia ugenini ni faida kubwa kwao, lakini kupajua mahali watakapocheza mapema itawasaidia kujiandaa na kuwaduwaza wapinzani wao hao aliodai msimu huu wana udhaifu mkubwa kwenye idara zao karibu zote.

“Sauzi sio mbali halafu kama Simba itacheza Johanesburg mazingira yapo, ikipangiwa Cape Town ni sawa na hapa, mechi yao wanaweza kuimalizia ugenini na ile ya marudiano ya nyumbani ikawa ni ya kukamilisha tu ratiba kujiandaa kucheza nusu fainali,” alisema Kawemba.