Vipigo vya Liverpool na Man Utd ni mchoko?

Thursday October 08 2020
man utd pic

 Usiku wa Jumapili iliyopita ulikuwa na majanga kwa klabu za Liverpool na Manchester United katika Ligi Luu England baada ya kupokea vipigo vya kustusha. Siku hiyo Man Utd ilichezea kichapo cha mabao 6- 1 kutoka kwa Totenham kisha baadaye ilifuata Liverpool iliyochezea kipigo cha mabao 7-2 kutoka kwa Aston Villa.

Itakumbukwa Man Utd ilipambana sana msimu uliopita kufika tatu bora huku pia ikishiriki Kombe Europa. Hivyo ni dhahiri huenda pia kuna baadhi ya wachezaji wamechoka.

Kwa Liverpool wao walipigana kuhakikisha wanabaki kileleni na kutwaa ubingwa wa ligi. Vilevile walijaribu kupambana kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na wachezaji waliopambana kupata mafanikio hayo karibu asilimia 80 ni walewale, hivyo hoja ya kuchoka au kuwa na mchoko ina mashiko kitabibu. Pale mchezaji anapotumika sana na mara kwa mara ni kawaida kufikia mahali akachoka kimwili na kiakili.

Viungo vya mwili huwajibika kufanya vitendo mbalimbali uwanjani ikiwamo kukimbia, kuruka, kupiga mpira, kunyumbulika na kupiga chenga. Vitendo hivyo vinahitaji mwili ambao ni timamu kimwili na kiakili kuweza kutenda, hivyo mtetereko wa aina yoyote katika maeneo hayo huwa na matokeo hasi kiutendaji.

Mfano mchezaji ambaye amechoka kimwili hata uwezo wake kiakili uwanjani unapungua ikiwamo pale anapotakiwa kufanya uamuzi sahihi au umakini katika kucheza.

Advertisement

Mchoko unaweza kumfanya mchezaji kuwa mvivu na kufanya mambo ya ajabu uwanjani ambayo yanaweza kuigharimu timu kufungwa kizembe.

Mfano halisi ni kitendo cha Anthony Martial kufanyiwa rafu na kuamua kumrudishia mpira mchezaji wa Spurs kiliigharimu Man Utd kwani alilimwa kadi nyekundu na kusababisha wacheze pungufu hata kabla ya kipindi cha pili.

Kitendo hicho kinatoa picha kuwa umakini wake kiakili ulikuwa na mtetereko kwani angekuwa makini angekumbuka kuwa kurudishia faulo huzaa kadi nyekundu.

Hata kwa mlinda mlango bora wa Liverpool, kitendo cha kukosa umakini wakati anamrudishia beki wake wa kulia mpira kulichangia kufungwa bao la kwanza kirahisi.

Mchezaji anapokuwa amechoka au kuwa na uchovu usioisha kutokana na kutumika sana hupoteza hata ile ari na hamasa ambayo alikuwa ameibeba ili kuisaidia timu yake kushinda.

Unaweza kuwa na kiwango kikubwa na mwili shupavu lakini ukipoteza tu ari na hamasa matokeo yake ni kutokuwajibika vyema uwanjani.

Je nina kifanyike kuepukana na mchoko?

Wachezaji wote wameathirika kiakili na vipigo vile vya aibu, kiasi kwamba hata wakati wanaelekea katika vyumba vingine wapo ambao hawakutaka hata kupeana mikono.

Hapo inahitajika tiba ya kisaikolojia ili kuweza kuwaweka sawa kiakili wachezaji hawa. Kitabibu tiba hii inaitwa Psychotherapy inaweza kufanywa na Daktari, Mwanasaikolojia au Mshauri nasaha.

Klabu ya Liverpool ni moja ya klabu barani Ulaya ambayo ni maarufu kwa kuwatumia sana wanasaikojia kuweza kusahihisha mtetereko wa kiakili wa wachezaji wao.

Jopo la ufundi linahitajika pia kufanya tathimini ya mazoezi na mafunzo wanayotoa kwa wachezaji kama hayazidi kiwango kwani mazoezi makali yanaweza kumchosha mchezaji na kumpa mchoko.

Vile wachezaji binafsi anapaswa kujitathimini kwa upande mazoezi yake binafsi na utimamu wake kimwili. Yapo mazoezi ya ziada yasiyo na kipimo yanaweza kuichosa misuli ya mwili.

Utimamu wa mwili wake unaweza kuathiriwa na mienendo mibaya ya kimaisha ikiwamo unywaji na uvutaji tumbaku. Mambo haya yote yanaweza kuchangia mchezaji kuwa na mchoko.

Mchezaji atahitajika kutotumia vitu hivi ili kulinda utimamu wake wa kimwili na kiakili.

Kulala na kupumzika ni jambo la msingi sana kwa mchezaji kuondokana na mchoko. Angalau mchezaji alale masaa 6-8 kwa usiku mmoja na pia kupumzika maeneo tulivu na yenye hewa yakutosha masaa 2-3.

Kunywa maji mengi mara kabla na baada ya mazoezi au mechi angalau anywe lita 2-3 na pia kutumia matunda yenye maji maji mengi.

Lishe yenye protini nyingi itahitajika kutumiwa sana na wanamichezo ambao wana mchoko kwani lishe hii ndiyo inayojenga mwili hatimaye kuponya mchoko.

Misuli inapofanya kazi huweza kuwa na mchoko kutokana na mrundikano wa taka ambazo huwa ni zao baada ya matumizi ya sukari ya mwili.

Walimu wanatakiwa kutathimini aina ya mazoezi wanayowapa wachezaji wao na pia kutumia mtindo wa kuwabadili kikosi cha kwanza ili kuzuia kutumika sana na kupata mchoko. Usingaji wa mwili wa mchezaji pamoja na mazoezi tiba laini ni moja ya njia muhimu za kumaliza hali ya mchoko na kusaidia misuli yenye vijeraha na kupona.

Hali ya mchoko inaposhindikanika kuondoka kwa njia hizi ni vizuri kufika katika huduma za Afya kwa ushauri na uchunguzi zaidi.

 

Advertisement