Vipigo viendelee tu!

Muktasari:

VIPIGO viendelee. Ndio kaulimbiu ya Simba wote waliopo jijini hapa kuwakabili Kaizer Chiefs usiku wa leo kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba wana hamu ya kuvunja rekodi ya 1974 na kuvuna kitita kikubwa cha fedha. Mechi itapigwa leo saa 1.00 usiku za Tanzania sawa na saa 12 za hapa.

VIPIGO viendelee. Ndio kaulimbiu ya Simba wote waliopo jijini hapa kuwakabili Kaizer Chiefs usiku wa leo kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba wana hamu ya kuvunja rekodi ya 1974 na kuvuna kitita kikubwa cha fedha. Mechi itapigwa leo saa 1.00 usiku za Tanzania sawa na saa 12 za hapa.

Mchezo huo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambao itacheza kwenye Uwanja wa FNB ni muhimu kwa Simba kukamilisha hesabu kabla ya kuja kuzifunga nyumbani mwishoni mwa wiki ijayo.

Matokeo mazuri katika mchezo wa leo utakaochezeshwa na refa Sidi Alioum kutoka Cameroon, yatathibitisha Simba ina kiu ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa msimu huu baada ya kuanza kuonyesha dalili kwa kufanya vyema hatua ya makundi ambapo waliongoza wakiwa na pointi 13, wakifunga mabao tisa na kuruhusu kufungwa mawili.

Mbali na hilo, Simba inafahamu ina deni la ama kufikia au kuvunja rekodi ya 1974 ambapo walitinga nusu fainali na kutolewa na timu ya Mehalla Kubra ya Misri kwa penati baada ya mechi mbili kumalizika mabao 3-3.

Ukiondoa mafanikio hayo, kufanya vizuri kutaiweka katika nafasi nzuri ya kujihakikishia Dola 875,000 ambazo kila timu inayotinga nusu fainali inapewa na CAF. Ni mkwanja mwingi sana.

Ndani ya uwanja Simba wanapaswa kucheza kwa nidhamu na tahadhari ili kukabiliana na ubora wa Kaizer Chiefs na kunufaika na udhaifu wa wapinzani wao. Uimara wa kiufundi wa Kaizer Chiefs ni uwezo wa kutumia mipira ya krosi na kona ambayo imekuwa silaha kubwa kusaka mabao.

Nyota wa timu hiyo wamekuwa wakionyesha uwezo mkubwa kumalizia mipira ya kona au krosi wanaposhambulia, hivyo safu ya ulinzi ya Simba inapaswa kuwa makini katika hilo. Katika mabao matano ambayo Kaizer Chiefs imefunga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, matatu yametokana na mipira ya krosi na kona, moja likiwa la penati na lingine moja pasi ya kupenyeza katikati.

Pia kingine kinachoibeba Chiefs ni uwezo wa baadhi ya nyota wanaocheza safu ya kiungo na ulinzi kufunga mabao wanapoenda mbele kusaidia mashambulizi.

Ukiwaondoa Bernard Parker na Khama Billiat ambao kila mmoja amepachika bao moja hatua ya makundi, hakuna washambuliaji wengine waliofunga ambapo mabao mengine matatu yamefungwa na mabeki Erick Mathoho, Daniel Cardoso na kiungo Happy Mashiane. Pamoja na uimara wao huo, Chiefs wana udhaifu ambao kama Simba watautumia vyema, wanaweza kumaliza shughuli ugenini. Safu yao hasa mabeki wa kati imeonyesha udhaifu kucheza mipira ya juu kwa vichwa hasa ile ya krosi, jambo ambalo limekuwa likiwapa mwanya wapinzani wao kuwaadhibu.

Lakini mbali na hilo, Chiefs wamekuwa na tatizo katika ukabaji ambapo walinzi wamekuwa wakiwapa uhuru wapinzani kuwa na mpira jirani na eneo lao la hatari na hivyo kuwapa nafasi ya kufanya uamuzi pale wanaposhambulia.

Udhaifu wa washambuliaji wao kutumia nafasi wanazotengeneza kufunga mabao, ni neema inayoweza kuibeba Simba ikiwa wapinzani wao hao watashindwa kufanyia kazi changamoto hiyo kwa muda uliobakia.

Hapana shaka Simba wataingia wakiwa hawana presha kubwa ya kucheza ugenini kutokana na matokeo waliyoyapata katika mechi za ugenini katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini pia hata takwimu zisizovutia za wenyeji wanapocheza katika Uwanja wa FNB.

Msimu huu katika mechi tano ambazo Simba imecheza ugenini, imeibuka na ushindi mara mbili, sare moja na kupoteza mbili, ikifunga mabao mawili na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.

Kwa upande wa pili, Kaizer Chiefs wamekuwa na nuksi wanapoutumia uwanja huo kwani katika mechi 26 ilizocheza nyumbani msimu huu imeibuka na ushindi mara sita, sare 12 na kupoteza nane.

Imefunga mabao 23 tu ikiwa ni wastani wa bao 0.88 kwa kila mchezo ikifungwa mabao 26, ikiwa ni wastani wa bao kila mchezo. Kwenye Ligi ya Mabingwa pekee, wameibuka na ushindi mara mbili kati ya mechi tano walizocheza, wakitoka sare tatu, wakifunga mabao matatu ikiwa ni wastani wa bao 0.6 kwa kila mechi ingawa haijaruhusu bao.


Makocha

Makocha wa timu zote kila mmoja ameonyesha kucheza kwa tahadhari ingawa wamejinasibu kupata matokeo mazuri.

“Ni mechi ngumu kwani Simba imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano haya. Imeifunga timu kubwa ya Al Ahly, hivyo hatupaswi kuidharau na kuibeza. Hata hivyo tumejiandaa vizuri kukabiliana nayo.

“Tumekuwa na changamoto ya ratiba na majeruhi lakini tupo tayari kwa mchezo na tuna imani tutafanya vizuri,” alisema kocha wa Kaizer Chiefs, Gavin hunt.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema wamejipanga na watatumia mbinu zilezile walizotumia kule DR Congo na Sudan.“Mchezo huu ni muhimu kuandika historia mpya kwa soka la Tanzania na kundi hili la wachezaji. Simba siku zote imekuwa ikicheza mpira, lakini katika mechi hii tutacheza kwa tahadhari na nidhamu kubwa katika kujilinda na kushambulia pale tutakapolazimika kufanya hivyo.

“Wachezaji wangu wanafahamu nini wanachotakiwa kufanya na tunaamini tunaweza kufanya vizuri hapa,” alisema.

Kikosi cha Simba katika mchezo wa leo kinaweza kupangwa hivi: Aishi Manula, Mohamed Hussein, Kapombe, Wawa, Onyango, Taddeo, Luis Miquissone, Mkude, Mugalu, Chama na Bwalya.