VIDEO: Manara amuomba radhi Karia, akiri kukosea

Manara amuomba radhi Karia, akiri kukosea

Muktasari:

  • Msemaji wa Yanga, Haji Manara amemuomba radhi rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kwa majibizano wakati wa mechi ya fainali ya FA kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Msemaji wa Yanga, Haji Manara amemuomba radhi rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kwa majibizano wakati wa mechi ya fainali ya FA kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Amesema kwa umri na hadhi ya urais, alipaswa kuwa na busara zaidi ya aliyoitumia wakati wa tukio hilo.

"Nilikosea kujibizana na rais na ninaomba radhi," amesema Manara leo na kufafanua.

"Jana nilienda kumuona rais wa TFF nyumbani kwake, tulipiga picha, kunywa juisi ya pamoja na kumuomba radhi juu ya kilichotokea".

"Tukio lile halikuwa na hata neno moja la tusi, sema ilinitokea katika midadi tu ya mchezo  na mimi uwa na presha ya mechi".

"Kwenye mechi ile nusu ya kwanza upande wetu palikuwa pagumu, nikawa najiandaa kuondoka nili nikaangalie mpira kwenye televisheni".

Manara amuomba radhi Karia, akiri kukosea

"Wakati nashuka, RC Mogella akaniita, tukawa tunasalimiana, nikasikia sauti ya rais kwa ukali ile kwangu ukuongeza na midadi ya mechi nilishindwa kui control".

"Lakini sikutamka tusi, nilimuuliza kuna kitu gani, wakati akinifokea, akasema wamesikia taarifa kuna mtu ameuwawa, hivyo wewe ondoka hapa, kama binadamu sikujisikia vizuri, mimi nahusikaje kwa huyo mtu".

"Nikamwambia unachokifanya sicho, nikaondoka eneo hilo, mpira ulivyoisha, rais alinisalimia tulipeana mkono tulipoenda kwenye medali, ingawa nilitaka nimtafute baada ya mechi," amesema.

Amesema jana alimwambia Injinia Hersi Said waende kumuona rais Karia kwani yeye ni  mdogo kwake.

"Nilimwambia rais nimekuja kukuomba radhi kwa kukujibu vile na kujibizana na wewe nilikosea, haijalishi wewe ndiyo ulianza, nisamehe".

Amesema kuomba kwake radhi haijalishi kwamba asiadhibiwe kama itaonekana ana hatia.