Ukuta wa Coastal mtegoni

Dar es Salaam. Udhaifu wa safu ya ulinzi ya Coastal Union unaweza kuwa fursa nzuri kwa washambuliaji wa Yanga kumaliza ukame wa mabao wakati timu hizo zitakapokutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini leo kuanzia saa 1.00 usiku.

Baada ya kusota katika mechi nne zilizopita ambazo washambuliaji wa Yanga walifunga bao moja tu, leo inaweza kuwa nafasi kwao kumaliza nuksi inayowaandama ikiwa safu ya ulinzi ya Coastal itaendelea kuwa na udhaifu ilioonyesha katika mechi nne zilizopita.

Katika mechi nne zilizopita ambazo Yanga imefunga mabao manne tu, moja katika kuila mchezo, ni bao moja tu lililofungwa na wachezaji wa safu ya ushambuliaji ambalo lililipachikwa na Michael Sarpong katika mechi yao ya kwanza waliyotoka sare ya bao 1-1 na Prisons lakini katika michezo iliyofuata mabao mawili yamefungwa na beki wa kati Lamine Moro na lingine moja likifungwa na kiungo Mukoko Tonombe.

Changamoto kubwa ambayo imeonekana kuwaathiri washambuliaji wa Yanga ni nafasi chache za mabao ambazo timu hiyo imekuwa ikitengeneza lakini pia hata utulivu na umakini kwao binafsi pindi wanapokuwa karibu na lango la timu pinzani.

Bahati nzuri kwao leo wanakutana na Coastal Union ambayo safu yake ya ulinzi imekuwa ikiyumba na kwa kiasi kikubwa hilo linachangiwa na kukosa uzoefu kwa mabeki wake wa kati, Mwinyi Said, Peter Mwangosi, Martin Silvester, na Seif Bihaki jambo ambalo limepelekea wawe wanafanya makosa ambayo huwa yanaigharimu timu hiyo.

Katika kulithibitisha hilo, Coastal Union katika mechi za ke nne imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu dhidi ya Namungo FC, Azam FC, Dodoma Jiji FC na JKT Tanzania.

Mechi nyingine za leo :

Gwambina v Ihefu

Namungo v Mwadui

Mbeya City v Prisons