Twaha Kiduku:Promota amekimbia na pesa zangu ila...

Twaha Kiduku:Promota amekimbia na pesa zangu ila...

Muktasari:

Changamoto ya mabondia kudhurumiwa malipo yao baada ya mapambano ilikuwa imetoweka kabla ya kuibuka upya kwenye pambano la Twaha Kiduku na Mthailand.

Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) imesema itamburuta mahakamani promota Shomari Kimbau aliyeandaa pambano la Twaha 'Kiduku' Kassim na Sirimongkhon Iamthuam wa Thailand kwa madai ya kukimbia na pesa za mabondia.

Licha ya TPBRC kueleza hayo, Twaha Kiduku amesema hawezi kukubali promota huyo amdhurumu pesa zake, atapambana hadi mwisho ili kupata haki yake.

Kiduku alizichapa na Sirimongkhon Oktoba 30 kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba pambano la raundi 10 la uzani wa super welter ambalo awali Kimbau alieleza ni la ubingwa wa WBC, lakini ikawa tofauti siku ya pambano.

Baada ya pambano hilo baadhi ya mabondia akiwa Twaha Kiduku walipewa ahadi ya kulipwa ndani ya siku tano, ingawa hadi leo mabondia hao hawajalipwa.

"Nadai robo tatu ya pesa tulizokubaliana. Awali promota alinipa robo ya malipo yangu kwa makubaliano iliyobaki nitapewa siku ya pambano," amesema Kiduku.

Bondia huyo amesema wiki iliyopita walikwenda kwa promota akiwa na bondia mwingine wa uzani wa juu, Alphonce Mchumiatumbo ambaye pia anadai pesa zake, lakini hawakumkuta Kimbau nyumbani kwake.

"Simu hapokei, nyumbani kwake hayupo, ila ninachomwambia pesa yangu atanilipa atake asitake, ile ni haki yangu, nimefanya kazi nastahili kulipwa," amesema Kiduku.

Kimbau alipotafutwa kwa siku tatu mfululizo ili kujua hatma ya pesa za mabondia hao, simu yake iliita bila kupokelewa.

Rais wa TPBRC, Agapeter 'Mnazareth' Basil anasema anachokifanya promota huyo ni uhuni.

"Tumelifikisha suala hilo Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kilichobaki ni promota kukamatwa na kupelekwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake," amesema Agapeter.

Amesema kama Kamisheni tayari imemfungia mwaka mmoja promota huyo kutojihusisha na masuala ya ngumi, na wanaendelea kufuatilia suala hilo hadi pale mabondia watakapopewa haki zao.

"Tumejaribu kumtafuta promota mara kadhaa, nyumbani kwake hayupo na simu hapokei, ubabaishaji kama huu Kamisheni hatuutaki na niwahakikishie mabondia malipo yao kwenye pambano lile watayapata," amesema Agapeter.

By ImanI Makongoro