Tuzo za wanamichezo bora BMT zaiva

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga (wa tatu kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Tuzo za Wanamichezo ya baraza hilo kwenye uzinduzi wa tuzo za mwaka huu. 

Muktasari:

  • Faida kubwa kwenye utoaji tuzo ni kuchagiza maendeleo ya michezo ikiwemo kuongeza viwango vya wachezaji katika kupambana kutaka kuwa sehemu ya tuzo.

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), limeandaa tuzo za wanamichezo bora mwaka 2023 zinazotarajiwa kufanyika Juni 9, 2024 kwenye Ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki, Dar es Salaam.

Tuzo hizo ni mara ya pili kufanyika baada ya mwaka jana, Machi 17, 2023 kwenye Ukumbi wa Mlimani City.

Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga amesema dhamira ya hafla hiyo ni kuwaenzi na kuwaheshimisha wanamichezo kwa kufanya vizuri katika michezo ya kanda, Afrika na kidunia.

Amesema kuna faida kubwa kwenye utoaji tuzo ni kuchagiza maendeleo ya michezo ikiwemo kuongeza viwango vya wachezaji katika kupambana kutaka kuwa sehemu ya tuzo.

“Tunatoa tuzo kwa wanamichezo wanaofanya vizuri ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuipeperusha vyema bendera ya Taifa. Sasa hivi nchi yetu sio kichwa cha mwendawazimu kwa sababu timu zote zimejipamga," amesema Tenga.

"Ni miaka mingi sana kuona timu mbili kuingia robo fainali (Ligi ya Mabingwa Afrika) kama ilivyo kwa Simba na Yanga. Hii kazi nzuri kwa uongozi, makocha na wachezaji.”

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Mkumbukwa Mtambo amesema safari hii kuna tofauti na mwaka jana, kwani mwaka jana kila mchezo uliofanya vizuri ulipewa fursa ya kuwa na mchezaji bora ambapo kwa mwaka huu zitakazotolewa ni tuzo za ujumla na sio kwa kila mchezo.

“Mabadiliko haya yanalenga kuongeza ushindani na ufanisi ikiwa ni pamoja na kuleta usawa wa uthamani kwa michezo yote. Kadhalika mabadiliko haya yataongezea thamani tuzo hizi," amesema Mtambo.

"Kuongezeka vipengele vingine ambavyo kwa mwaka jana havikuwepo. Baadhi ya vipengele vilivyoongezeka ni pamoja na kocha bora wa mwaka, mwamuzi bora wa mwaka na lengo ni kuendelea kuhakikisha kuwa wadau wote muhimu katika tasnia ya michezo wanathaminiwa na kutambuliwa.”

Ameongeza kuwa mabadiliko ya vipengele vya tuzo yamefanyika ili kuendelea kuzipa thamani zinazotolewa pamoja na kuongeza ushindani baina ya wanamichezo anaopewa tuzo wawe ni wale ambao wamekuwa na mafanikio zaidi kuliko wengine.

Amesema katika kuhakikisha kuwa mchakato wa utoaji tuzo unafanyika kwa uwazi, weledi na umakini mkubwa vyama na mashirikisho yote ya michezo yameshirikishwa katika uteuzi wa wanamichezo bora kwenye michezo yao.

Ameeleza kuwa Kamati ya Tuzo imepokea mapendekezo ambayo itayachambua na kuchagua wanamichezo bora waliokidhi vigezo vilivyowekwa katika vipengele mbalimbali, ikiwemo mwanamichezo bora wa kiume na kike wa mwaka.

Vipengele vingine ni mwanamichezo bora kijana wa kiume na kike, mwanamichezo bora wa kiume na kike mwenye ulemavu (kwa upande wa klabu), timu bora (upande wa zile za  Taifa) na kocha bora wa kiume na kike.

Ametaja vipengele vingine ni mwanamichezo bora wa kiume na kike kutoka mashindano ya shule, mwamuzi bora wa kiume na kike wa mwaka pamoja na mwanahabari za michezo bora wa kiume na kike.