Tshishimbi: Simba mziki mnene

NAHODHA wa zamani wa Yanga, Papy Tshishimbi amesema pambano la watani wa jadi litakalopigwa leo Mei 8 saa 11:00 jioni timu itakayokuwa imefanya maandalizi itakaibuka na ushindi, lakini kaongeza kuwa Simba ya sasa mziki wake ni mnene na Yanga lazima ijipange.

Simba na Yanga zinavaana kwenye pambano la 106 katika Ligi ya Bara tangu 1965, huku Jangwani wakiwa vinara kwa kushinda mara 37 dhidi ya 31 za Msimbazi na mechi 37 zikiisha kwa sare, lakini timu zote zikiwa kwenye vita ya kuwania ubingwa Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka DR Congo, Tshishimbi anayekipiga AS Vita, alisema amekuwa akifuatilia kwa karibu timu hizo na kwa kulinganisha vikosi hivyo, Simba wako bora zaidi ya Yanga kutokana na mafanikio iliyopata mfululizo katika michuano ya ndani na kimataifa.

“Yanga sio kama wapo vibaya. Hapana! Ila ni kwamba timu haijatulia na imekosa utulivu, lakini wana uwezo wa kuwapa ushindani wa kutosha Simba kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza ulioisha kwa sare ya 1-1,” alisema.

“Mtazamo wangu haitakuwa mechi rahisi kwa Simba au Yanga kwani wote wawili wanapambania ubingwa na yule ambaye atapoteza huenda akajiongezea ugumu. Ila kwa aina ya vikosi, Simba wapo vizuri. Hata hivyo mara nyingi timu kubwa zinapokutana hata kama kuna moja haipo vizuri inakuwa tofauti ila ile ambayo itashinda inatokana na kufanya maandalizi ya kutosha pamoja na bahati.”

Tshishimbi alikuwa kwenye kikosi kilichoifunga Simba bao 1-0 katika Ligi Kuu Bara mechi iliyopigwa Machi 8, 2020, mfungaji akiwa ni Bernard Morrison.

Hata hivyo, nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema mechi hiyo mara zote huwa ngumu licha ya kwamba kunaweza kuwepo moja ya timu kuonekana haifanyi vizuri wakati huo.

Chambua alisema wakati huu Yanga hawapo imara, lakini wanaweza kubadilika katika mchezo huo dhidi ya Simba mpaka wakashangaza mashabiki wengi wa soka.