TFF: Tumewasikia, tutarekebisha

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kumbe limesikia manung’uniko ya wadau wa soka juu ya kutoridhishwa na baadhi ya washindi waliopewa tuzo walizoziandaa kwa msimu uliopita zilizotolewa majuzi na kusema watarekebisha dosari zilizojitokeza.

Hafla ya tuzo hizo ilifanyika Alhamisi jijini Dar es Salaam na kuna baadhi ya vipengele vililalamikiwa kwa madai washindi hawakustahili, pia tuzo zenyewe ni kama ziliandaliwa kizimamoto kiasi hata uteuzi wake kuonekana umejaa ubabaishaji kuliko uhalisi wa tuzo zenye hadhi kama hizo.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za TFF, Ahmed Mgoyi alisema wamepokea maoni mbalimbali kuhusu tuzo hizo baada ya kutokea kwa malalamiko na watayafanyia kazi tuzo zijazo.

“Hizi ni tuzo za kwanza kwa TFF. Nakiri tumekutana na changamoto kadhaa na tumekabiliana nazo, lakini hata sisi kama kamati tuna maoni tofauti, japo tunafikia muafaka hadi wote tuwe kitu kimoja,” alisema.

“Hatujali maoni yanatolewa kwa njia gani na muwasilishaji anayatoa kwa namna ipi, bali tutaweka vigezo vitakavyotumika kumpata mshindi kwa kila tuzo husika, ili kuondoa dosari zilizojitokeza.”

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza aliyeteuliwa kuwania tuzo ya Kocha Bora na kubwagwa na Didier Gomes wa Simba, aliwapongeza washindi akishauri kuwe na zawadi za nyongeza.

“Kila jambo halikosi kasoro. Niwapongeze TFF, ila kitu nachopenda kuwashauri tuzo zisiishie tu kuwapa tuzo zenye nembo fulani, bali kuwe na kiasi cha fedha kinachowekwa wazi lengo ni kuongeza motisha zaidi,” alisema Baraza aliyeshindanishwa pia na George Lwandamina wa Azam FC.

Vipengele vilivyolalamikiwa ni Mchezaji Bora wa Mwaka aliyopewa John Bocco badala ya Clatous Chama ambaye wadau waliona anastahili, huku Mchezaji Bora wa ASFC ikienda kwa Feisal Salum wa Yanga badala ya Luis Miquissone anayedaiwa kustahili.

Pia tuzo ya Mhamasishaji Bora wa Mwaka aliyopewa Bongo Zozo ikilalamikiwa akitajwa Haji Manara aliyekuwa Simba (sasa Yanga) kuwa alistahili.

Kadhalika tuzo ya Mchezaji Chipukizi aliyopewa Abdul Suleiman ‘Sopu’ inaelezwa hakustahili kwani amecheza Ligi Kuu tangu 2017. TFF ilitoa tuzo zaidi ya 25, kwa wachezaji, kocha na maofisa wengine waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2020/21.