TFF, Bodi ya Ligi walaani vurugu za mashabiki Yanga kwa Simba

Monday September 28 2020
tff pic

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) na uongozi wa Simba wametoa onyo kwa mashabiki wa soka wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa amani katika soka.

Kauli za viongozi hao wa Soka hapa nchini zimetolewa baada ya jana mashabiki wa Yanga kuwafanyia fujo mashabiki wa Simba katika uwanja wa Jamhuri ambapo Yanga ilikuwa ikimenyana na Mtibwa Sugar na kushinda bao 1-0.

TFF imekemea kitendo hicho kisichokuwa cha kiungwana kilichofanywa na mashabiki hao, huku ikilaani kwa madai vinaweza kuleta uvunjifu wa amani katika viwanja vya michezo.

"Vitendo hivyo havina nafasi katika mpira wa miguu na vinapaswa kukemewa na kila mpenda soka, tunaamini vyombo vya usalama vitachukua hatua stahiki kwa waliohusika na uvunjifu huo wa amani," ilisema taarifa hiyo kutoka TFF.

Kwa upande TPLB kupitia kwa Mtendaji wake Mkuu Almas Kasongo amesema, hawatakubali kuona vitendo vya namna hii vinajitokeza katika soka na kusababisha uvunjifu wa amani.

Kasongo alisema, watawachukulia hatua zaidi klabu ambazo mashabiki wao wanafanya vurugu kama ambavyo mashabiki wa Yanga walivyofanya katika mchezo wa jana.

Advertisement

"Hata sisi bodi ya ligi hatujapendezwa hata kidogo na kilichofanywa na mashabiki hao, mpira sio uadui hivyo basi tutadili na klabu husika ambayo wanachama wake watafanya vitendo hivyo,"alisema Kasongo.

''Kanuni ya bodi ya ligi inasema mchezo wa kiungwana inawahusu hadi mashabiki sio wachezaji tu, kanuni ya 45 imeelezea namna ambavyo klabu itaadhibiwa kwa wanachama wake na mashabiki kufanya fujo,'' alisema Kasongo.

Kwa upande wao Simba kupitia kwa Mkuu wao wa Idara ya Habari ya klabu hiyo, Haji Manara amewataka mashabiki na wanachama wao kutothubutu kulipa kisasi kutokana na vitendo vinavyoendelea juu yao dhidi ya watani zao Yanga.

"Hatuwapangii TFF na Bodi ya Ligi cha kufanya ila hivi vitendo athari yake ni kubwa zaidi, kama Simba tumechukizwa na kitendo hicho kilichofanywa na mashabiki wa Yanga Morogoro, tunawaomba Simba wasifanye visasi vya aina yoyote katika hili,"

"Mpira ni starehe ni burudani, mpira ndio kitu kinachounganisha watu bila ya kujali itikadi dini wala kabila tusilipe kisasi tusithubutu hata kidogo Simba sisi wastaarabu, na wala tusionyeshe dalili ya aina yoyote ya kisasi,"alisema Manara.

 

 

 

Advertisement