Tanzania yakwaa kisiki wavu Afrika

Muktasari:

  • Timu hiyo itacheza mechi yake ya mtoano kesho Alhamisi Aprili 22, 2021 saa 10 jioni kwa saa za Tanzania kutafuta nafasi ya tisa hadi 16.

Tanzania imeshindwa kufuzu kucheza robo fainali kwenye mashindano ya wavu ya klabu bingwa Afrika yanayoendelea mjini Tunis, Tunisia.

Klabu ya Mwanza Transit Camp (MTC) inayoiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo imekosa tiketi hiyo baada ya kumaliza ya tatu kwenye kundi C.

Timu hiyo ilihitaji ushindi wa kuanzia seti 2 au zaidi kwenye mchezo wao wa mwisho wa makundi dhidi ya wenyeji, club Olympique de Kelibia ili kufuzu imechezea kipigo cha seti 3-1.

Katika seti ya kwanza Tanzania ilifungwa pointi 25-14 na 25-21 seti ya pili kabla ya kubadili upepo seti ya tatu kwa kushinda pointi 25-18, ingawa ilichapwa kwenye seti ya nne kwa pointi 25-20.

Kabla ya mechi hiyo, Tanzania iliichapa Wolaita Dicha ya Ethiopia seti 3-1.

Katibu Mkuu wa Chama cha mpira wa wavu Tanzania (Tava),
Alfred Serengia alisema wawakilishi hao wa Tanzania wamepoteza mechi hiyo kutokana na uzoefu.

"Tumefungwa mechi mbili na kushinda moja, matokeo ambayo hayajatupa nafasi ya kufuzu robo fainali, japo hatujatolewa mashindanoni," amesema Serengia.

Amesema timu hiyo itacheza kesho Alhamisi mechi ya kutafuta timu itakayomaliza mashindano hayo katika nafasi ya tisa hadi 16.

Katika mechi ya kwanza, Tanzania ilichapwa na Nemostar ya Uganda kwa seti 3-2 za pointi 15-25, 22-25, 25-21, 25-11 na 11-15 kabla ya kupindua meza na kuifunga Ethiopia na jana kuchapwa na wenyeji Tunisia.