Tanzania Prisons yapewa mbinu kuiua Yanga

TANZANIA Prisons imesema imeuangalia vizuri mchezo wa Yanga dhidi ya Ihefu na kubaini udhaifu ulipo kwa bingwa huyo mtetezi, hivyo mchezo wao dhidi ya Yanga Desemba 4 lazima wapige kwenye ‘mshono’.

Yanga ilipoteza dhidi ya Ihefu na kulala mabao 2-1 ikiwa ni mechi yake ya kwanza kupoteza katika misimu miwili mfululizo ya Ligi Kuu na sasa wanarejea Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuwakaribisha Tanzania Prisons.

Timu hizo zinakutana katika uwanja huo ikiwa msimu uliopita zilimaliza dakika 90 bila kufungana, hivyo kufanya mechi hiyo kuwa na upinzani mkali ikizingatiwa kila upande unataka pointi tatu.

Prisons katika mechi sita za nyuma haijaonja ushindi wowote ikiwa ni sare tatu na kupoteza idadi hiyo akiwa nafasi ya 11 kwa pointi 14 baada ya michezo 14, huku Yanga ikiwa na pointi 32.

Kocha Shaaban Mtupa alisema walitumia dakika 90 zote kuwasoma wapinzani hao na waliona mapungufu na Jumapili wanaenda kutonesha tena.

Alisema kwa sasa benchi la ufundi linaendelea kusuka kikosi chake kuhakikisha wanamaliza mzunguko wa kwanza matokeo mazuri huku akieleza kuwa watakuwa makini sana.

“Tumebaini wanafungika, tunaendelea kuwafua vijana kuhakikisha wanapitia mulemule kama Ihefu, japo tunafahamu mechi itakuwa ngumu na nzuri,” alisema Mtupa.

Alisema sehemu waliopo si salama lazima wapambane kupata pointi tatu ili kujiweka pazuri.