Tanzania Prisons yaitishia nyau Yanga

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Kazumba ni kama ameipiga mkwara Yanga baada ya kusema walikuwa wanatamani kukutana na Yanga katika hatua ya 16 bora kwenye Kombe la FA na kweli wamefanikiwa.

Tanzania Prisons ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Sahare Stars, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Abeid, Arusha, na kuwafanya wasonge kwenye hatua 16 Bora.

Kazumba, kabla ya mchezo wao na Sahare, alisema walipojua tu kwamba watacheza na Yanga kama watapata ushindi, jambo hilo liliwaongezea morali kwani wanawatamani.

“Wachezaji wangu walipojua tutacheza na Yanga kama tutaibuka na ushindi na kusonga mbele, morali yao iliongezeka na sasa wamefanikiwa kukutana nao kwenye mchezo ujao,” alisema kocha huyo msaidizi.

Kazumba alisema wanataka kulipa kisasi baada ya mchezo wao wa kwanza kupata sare ya 1-1 (Kwenye Ligi Kuu), hivyo anataka wapate ushindi katika mchezo huu na kusonga mbele.

“Tunawatamani sana Yanga, katika watu tunaowatamani ni wao kwa sababu wanacheza sana mpira, wanakuja nyumbani na tuliwakosa raundi ya kwanza baada ya kusawazisha, tutakutana nao mchezo ujao wa Kombe la FA,” alisema.

Kazumba aliongeza kwa kusema haoni ubora wa timu ya Yanga mbele ya kikosi chake cha Prisons hasa kuna utofauti kwenye mpira wao na wapinzani.

“Safari hii wakija ni mbili au tatu zitawahusu mbele yetu,” alijigamba kocha huyo.

Yanga ilitinga katika hatua hiyo baada ya kuichapa Kengold ya Mbeya kwa bao 1-0, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze alisema vijana wake wanahitaji kutwaa taji hilo msimu huu na watahakikisha kuwa wanashinda katika kila mcheo hadi fainali.

“Tunahitaji kila kombe, tumeanza na Kombe la Mapinduzi, tunahitaji kuendelea kufanya kazi zaidi uwanjani kwa ajili ya matokeo mazuri,” alisema Kaze.

Hatua ya robo fainali katika Kombe la Azam inatarajia kuchezwa Aprili 3 hadi 4, huku Yanga wao wakiifata Prison katika uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.