Tamu na chungu ushangiliaji wa kuruka sarakasi

Muktasari:

STRAIKA wa zamani wa Manchester United, Luis Nani alipenda sana kuruka sarakasi kila anapofunga bao na ilikuwa starehe yake kubwa iliyowafanya hata mashabiki kufurahia staili hiyo ya ushangiliaji.

STRAIKA wa zamani wa Manchester United, Luis Nani alipenda sana kuruka sarakasi kila anapofunga bao na ilikuwa starehe yake kubwa iliyowafanya hata mashabiki kufurahia staili hiyo ya ushangiliaji.

Ukiachana na Nani, mshambuliaji wa zamani wa Inter Milan na timu ya Taifa ya Nigeria, Obafemi Martin alikuwa kila akifunga bao furaha yake kubwa ilikuwa kushangilia kwa sarakasi za nguvu.

Nani na Martin ilikuwa ni mara chache sana kufunga bao pasipo kushangilia kwa sarakasi.

Kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson ilielezwa aliwahi kumpiga marufuku Nani kuruka sarakasi kwa kuhofia anaweza kuumia.

Licha ya kuwa ni furaha yao lakini ushangiliaji huo pia umekuwa burudani kubwa kwa mashabiki wa soka ambao hupenda kutazama wachezaji wakiruka ‘sambasoti’ hizo kila wanapofunga.

Hapa Bongo baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipenda kuruka sarakasi wanapofunga mabao yao akiwemo kiungo -mshambuliaji wa Dodoma Jiji, David Ulomi.

Lakini pamoja na staili hiyo ya ushangiliaji kupendwa na baadhi ya wachezaji, kuna wakati wanaweza kuumia na kuwaletea madhara makubwa wakiruka vibaya na kudondoka. Hivi karibuni katika mchezo wa Ligi Kuu, straika wa Mbeya Kwanza, Chrispin Ngushi aliwahishwa hospitali baada ya kudondoka baada ya kuruka sarakasi wakati akishangilia bao la kusawazisha la 2-2 dhidi ya Mbeya City.

Ngushi aliruka vizuri kwa ustadi mkubwa sarakasi hizo pasipo tabu yoyote, lakini sekunde chache baadaye wakati wenzake wanashangilia bao ghafla alidondoka na kufanya watoa huduma ya kwanza kumuwahisha hospitali kwa matibabu.

Mwanaspoti limezungumza na watu mbalimbali wakiwemo kocha, daktari, wachezaji na mashabiki kuhusu ushangiliaji huo

Ulomi Humwelezi kitu

Ulomi ambaye hupenda kushangilia kwa staili hiyo anaeleza utamu wake wa aina hiyo ya ushangiliaji.

“Kwangu ni ngumu sana eti nifunge bao halafu nishangilie kwa kawaida, haiwezekani ni lazima niruke sarakasi, pale ndio nakuwa na furaha ambayo iko moyoni ..nikifanya vizuri huwa najisikia vizuri tu kiafya.

“Ila wakati naruka nakuwa makini kwa sababu ukikosea kidogo tu basi unaweza kuumia vibaya, hivyo kabla sijaruka nawaandaa wachezaji wenzangu wasogee mbali kidogo maana huwa inahitaji uwe na nafasi ya kukuweza kuruka pasipo kuwepo mtu au kitu chochote mbele yako,” anasema.

Anatoa tahadhari kwa wachezaji wenzake kuwa kama hufanyii mazoezi kuruka sarakasi wasifanye hivyo kwani ushangiliaji huo ni hatari.

“Tangu nacheza chandimu nikiwa mdogo kabisa nilikuwa nikifunga bao lazima niruke sarakasi. Niwaombe sana wachezaji wenzangu wasiige kabisa kushangilia kwa mtindo huu kama hufanyii mazoez.”

Straika wa Gwambina, Miraji Salehe anasema aliwahi kuruka sarakasi baada ya kufunga bao, lakini aliamua kuacha baada ya kuona amepata kizunguzungu.

“Ni staili nzuri sana ya ushangiliaji, lakini kwangu niliamua kuachana nayo baada ya siku moja kuhisi kizunguzungu kikali, baada ya kuruka nikaona isije ikaniletea shida badaye. Lakini kuna watu wanaruka sarakasi vizuri tu bila kupata shida yoyote,” anasema Salehe.

Daktari afunguka

Daktari wa timu ya Biashara United, Shabani Shija anawashauri wachezaji kuacha mara moja staili hiyo ya ushangiliaji kwa kuwa ina madhara makubwa.

Anasema urukaji sarakasi una madhara mbalimbali mojawapo mchezaji akiruka vibaya anaweza kuangukia shingo au mkono kitu ambacho kinaweza kumletea shida kubwa kiafya.

Shija anasema pia kuruka sarakasi kunaweza kusababisha maumivu ya nyonga kwa mtu ambaye ana mazoezi ya urukaji.

“Kitendo cha kuruka sarakasi siyo kizuri kwa sababu kinaweza kusababisha kizunguzungu kikali. Wakati mwingine unaweza ukaruka vibaya na kufanya ukaanguka na kusababisha uumie na kufanya upate jeraha.

“Yule mchezaji wa Mbeya Kwanza aliruka vizuri kabisa, lakini sekunde chache baada ya kuruka alidondoka chini pale alipata kizunguzungu kikali ndio maana uliona ghafla amedondoka,” anasema Shija.

Kocha apiga marufuku

Kocha wa Copco Veteran inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Ahmed Simba anasema mwanzoni alikuwa hapendi kabisa staili ya ushangiliaji wa kuruka sarakasi kwa wachezaji wake lakini sasa amepiga marufuku kabisa.

Anasema amefanya hivyo baada ya kuona tukio la straika wa Mbeya Kwanza ambaye aliumia baada ya kuruka sarakasi.

“Kwanza hii aina ya ushangiliaji nilikuwa siipendi tangu mwanzo lakini sasa nimeamua kupiga ‘stop’ kabisa, nimewaambia wachezaji wangu kuna staili nyingi za kushangilia lakini sio hii na atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua za kinidhamu,” anasema Simba.

SHABIKI HUYU

Shabiki wa soka jijini Mwanza, Lushinge Mabolingo anasema huona burudani wachezaji wakishangilia mabao kwa staili mbalimbali hasa ya sarakasi.

“Hata Simon Msuva alikuwa anashangilia sana kwa staili ya kuruka sarakasi kwangu nilikuwa natamani afunge bao ili ashangilie kwa staili hiyo,” anasema Mabolingo.