Taifa Stars yaporomoka viwango FIFA

Wednesday April 07 2021
taifa pc

Kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars) wakiwa kwenye mazoezi.

By Charles Abel

Tanzania imeporomoka kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) vya mwezi Machi vilivyotangazwa leo

Licha ya Tanzania kuongeza pointi 1.05 kutoka zile 1087 ilizokuwa nazo hapo awali na kufikisha pointi 1088.05 katika viwango vya sasa, imejikuta ikiporomoka kutoka nafasi ya 135 hadi ile ya 137.

Kichapo cha ugenini cha bao 1-0 ambacho Taifa Stars ilikipata kutoka kwa Guinea ya Ikweta katika mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Matifa ya Afrika (Afcon) katika mechi baina yao iliyochezwa huko Malabo, Machi 25 kimeonekana kuchangia kuiangusha Tanzania katika viwango hivyo vya ubora vya mwezi Machi kwani kiliifanya ishindwe kufuzu mashindano hayo yatakayofanyika mwakani huko Cameroon licha ya kushinda kwa bao 1-0 katika mechi ya mwisho dhidi ya Libya.

Wakati Tanzania ikianguka kwa nafasi mbili, majirani zake Burundi wao wameporomoka kwa nafasi nne huku Rwanda wakipanda kwa nafasi nne.

Kufuzu Afcon kwa Ethiopia kunaonekana kumeibeba kwani imepanda kwa nafasi sita  kutoka ile ya 146 hadi ya nafasi ya 140.

Kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Uganda iliyo nafasi ya 84, ndio kinara licha ya kushuka kwa nafasi moja ikifuatiwa na Kenya (102), Sudan (123), Rwanda (129) wakati zilizo mkiani ni Eritrea (203), Somalia (197) na Djibout (183).

Advertisement

Senegal iliyo nafasi ya 22 kidunia, inaendelea kuwa kinara kwa upande wa Afrika licha ya kuporomoka kwa nafasi mbili, ikifuatiwa na Tunisia, Nigeria, Algeria na Morocco.

Hakukuwa na mabadiliko yoyote katika nafasi sita za juu kidunia kulinganisha na viwango vya ubora vya awamu iliyopita 

Ubelgiji imeendelea kuongoza ikifuatiwa na Ufaransa, Brazil, England, Ureno na Hispania

Advertisement