Straika mpya Simba atua nchini

SAA 7:45 mchana wa leo Jumamosi straika mpya wa Simba, Mnigeria Junior Lokosa aliwasili nchini akitokea kwao alipokuwa huko mara baada ya kumalizana na klabu yake ya zamani, Esperance Sportive de Tunis.

Lokosa mara baada ya kutua nchini alipokelewa na Mkuu wa Idara ya Uendeshaji, Dk. Arnold Kashembe ambaye alimsaidia kuweka mabegi yake katika gari aina ya Toyota Crown na baada ya hapo wakasepa zao.

Mwanaspoti ambalo lilikufichulia Simba kumuhitaji Lokosa, linafahamu mara baada ya kuondoka uwanja wa ndege walikwenda moja kwa moja katika ofisi za klabu hiyo ili kusaini mkataba na kupiga picha za utambulisho.

Mkataba huo ambao Lokosa amesaini ni wa miezi sita ambao atakuwa anaitumikia timu hiyo katika Ligi ya mabingwa Afrika mashindano ambayo wapo katika hatua ya makundi na Februari 12, wataanza kibarua hicho kwa kucheza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya AS Vita.

Lokosa kwa mara ya kwanza aliliambia Mwanaspoti kuwa amekuja nchini kuongeza uzoefu wake wa kucheza timu na mashindano makubwa katika klabu ya Simba ambayo inakiu ya kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya mabingwa Afrika.

"Ninao uzoefu wa kucheza mashindano haya makubwa lakini hata kucheza klabu kubwa kama Esperance Sportive de Tunis naimani hilo nitakuja kuliongeza katika timu hii ili kufanya vizuri," alisema.

"Ndio kwanza nimefika hapa nchini siwezi kusema mambo mengi ila muda ambao nitakuwepo hapa na mechi ambazo nitacheza kila kitu tutaona," alisema Lakosa ambaye akiwa na Esperance Sportive de Tunis msimu wa 2019-20, alicheza mechi 11 na kufunga mabao mawili.

Lokosa amezaliwa Agosti 23, 1993, alianza kucheza soka la ushindani katika klabu ya First Banka 2013-18, baada ya hapo alijiunga Kano Pillars 2018-19, akaitumikia mechi 35, na kufunga mabao 23, baada ya hapo ndio akajiunga na Esperance Sportive de Tunis lakini ametumika pia katika timu ya taifa ya Nigeria kuanza mwaka 2018.

Katika hatua nyingine wachezaji wote wa Simba ambao hawakuwa katika majukumu ya timu zao za taifa, jana jioni waliwasili kambini na kupata chakula cha usiku kwa pamoja kisha leo kuanza mazoezi kwa kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi, Ligi ya mabingwa Afrika na kombe la Simba.

Katika kuanza huko mazoezi leo Mwanaspoti linafahamu kocha mpya wa makipa, Mbrazil Milton Nienov ndio amekabiziwa mikoba ya kuwanoa wachezaji hao mpaka kocha mkuu atakapowasili nchini muda mchache kuanzia sasa.

Mwanaspoti ambalo lilikufichulia kuwa Simba wamemalizana na Milton na wengine wakafuatana lilipata taarifa zaidi kuwa Mbrazil huyo amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuwanoa makipa watatu wa Aishi Manula, Benno Kakolanya na Ally Salim.